Tuesday, February 2, 2016

Ukosefu wa mfumo wa kuondoa maji taka Shinyanga watishia kutokea mlipuko wa kipindupindu.

Katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga Bw.Abdul Dachi amemuagiza mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Shinyanga Eng.Sylvester Mahole kuhakikisha mfumo wa uondoaji wa maji taka katika mji huo unajengwa na kuanza kutumika haraka iwezekanavyo kwakuwa ukosefu wa miundombinu hiyo unachangia kutokea mlipuko wa magonjwa ya matumbo mara kwa mara ikiwemo ugonjwa wa kipindupindu.
Kauli hiyo imetolewa na katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga Bw.Abduli Dachi katika ziara ya kushtukiza aliyofanya katika ofisi za mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Shinyanga ambapo alibaini changamoto kadhaa zinazokwamisha mamlaka hiyo kutoa huduma bora kwa wananchi.
 
Katika hatua nyingine katibu Dachi ametembelea ofisi za bonde la maji kanda ya kati na kushtushwa na mrundikano wa vyuma chakavu na majengo yaliyochakaa katika eneo hilo ambapo alilazimika kutoa amri ya kuondolewa vyuma hivyo ili kupisha nafasi kwa ofisi za mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Shinyanga kuhamishia ofisi zake katika maeneo hayo.
 
Awali kabla ya maagizo ya katibu tawala mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mkoani Shinyanga Eng.Sylvester Mahole ameeleza baadhi ya changamoto zinazokwamisha mamlaka hiyo ikiwa ni pamoja na baadhi ya taasisi za serikali kutolipia ankara za maji na uhaba wa watumishi na vitendeakazi.
 

No comments:

Post a Comment