POLISI
mkoani Rukwa inamshikilia askari Magereza, Cleophas Chapaulinge kwa
kosa la kulewa na kupiga risasi hewani akiwa wodini katika Hospitali ya
Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga na kusababisha taharuki kubwa kwa
wagonjwa na wauguzi.
Kitendo
cha askari huyo kilizua taharuki kubwa kwenye wodi namba tisa ya
wanawake na watoto, ambapo akinamama walipiga mayowe kwa hofu huku
wakikimbia na kujificha kwenye chumba cha muuguzi wa zamu wakiwaacha
watoto wao vitandani.
Akizungumza
kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa lilitokea jana
alfajiri.
“Chanzo
ni ulevi wa kupindukia tulimpima kipimo kikaonesha kiwango cha ulevi
kilikuwa juu kupita kiasi alama zikiwa 300 huku kiwango cha kawaida cha
kipimo ni alama kati ya 70 na 40 …. Katika tukio hilo hakuna
aliyejeruhiwa na bunduki yake ilikuwa na risasi 10,” alisema.
Kamanda
Kyando alisema siku ya tukio, askari huyo akiwa na mwenzake walikuwa
kwenye lindo akilinda makazi ya Kamanda wa Magereza wa Mkoa, lakini
alitoroka lindo na kwenda hospitalini wodi namba tisa, ambako mkewe
alikuwa akimuuguza mwanawe aliyekuwa amelazwa hapo kwa matibabu.
Mke
wa mtuhumiwa huyo, Theresia Kalonga ambaye naye ni askari Magereza,
alikuwa amelazwa na mtoto wao wa kike mwenye umri wa mwaka mmoja na
miezi 10.
“Mtuhumiwa
huyo tunamshikilia huku taratibu za kumkabidhi kwa Kamanda wa Magereza
Mkoa wa Rukwa ili aweze kushtakiwa kwa taratibu za jeshi lao kabla ya
kufikishwa kwenye mahakama za kiraia, zinaendelea,” alisisitiza Kamanda Kyando.
Akizungumza
hospitalini hapo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk John Gurisha alisema
askari huyo baada ya kuingia wodini, aliweka silaha yake chini akafunua
chandarua na kuanza kuzungumza na mwanawe, kisha katoka nje na kufyatua
risasi hewani na kutoboa paa.
“Mtuhumiwa
huyo alizua kizaazaa kwani askari wetu waliokuwa lindo hapa hospitalini
walilazimika kukimbia ili kuokoa maisha yao baada ya kusikia mlio huo
wa risasi na kumuona askari huyo akielekea walipokuwa wamekaa,”
alisema na kuongeza kuwa askari huyo aliletwa hospitalini hapo na
mwendesha bodaboda ingawa hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa, lakini
alisababisha taharuki kubwa hospitalini.
“Askari
wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliwahi kufika hospitalini hapo na
kumtia nguvuni, na bunduki yake ilipokaguliwa ilikutwa ikiwa na risasi
kumi,” alisema.
Muuguzi
wa zamu wodini humo, Rose Katabi alisema askari huyo alipofyatua risasi
akinamama wodini humo walianza kupiga mayowe ya kuomba msaada huku
wakikimbia na kuwaacha watoto wao vitandani na kuvamia chumba cha
muuguzi kwa ajili ya kusalimisha maisha yao.
“Kwanza
kitendo cha kumuona askari huyo akiwa na silaha mkononi, mwili wangu
wote ulikufa ganzi nilihisi atatulipua kwa kutupiga risasi za moto
…aliiweka silaha yake hiyo chini na kuanza kuzungumza na mwanawe.
Aliniuliza kama mtoto wake ameshakunywa dawa, nikamjibu anakunywa dawa
mara moja usiku.
“Waliingia
walinzi wetu wawili wodini ndipo akaanza, kusema atarudi tena, akatoka
nje akiwa katikati ya mlango wa wodini alikoki bunduki yake na kufyatua
risasi hewani iliyotoboa paa kisha akaondoka na kutokomea gizani,” alisema.
Kwa
upande wa mke wa mshtakiwa huyo, Theresia alisema alipomuona na sare za
jeshi na silaha mkononi alimtaka arudi mara moja kazini.
Walinzi
waliokuwa kwenye lindo katika lango kuu la kuingia hospitalini hapo kwa
masharti ya kutoandikwa majina yao , walidai kuwa askari huyo
alifikishwa hospitalini hapo kwa usafiri wa bodaboda.
“Alitutia
shaka baada ya kukataa kusimama, kwani alipitiliza moja kwa moja akiwa
na silaha mkononi, tulijawa na hofu kubwa tukaamua kumfuata kwa nyuma
hadi akaingia wodi namba tisa alikolazwa mkewe na mtoto wake. Lakini
tulipomuona akikoki bunduki yake tulilazimika kukimbia na kwenda
kujificha ndipo tukasikia mlio wa risasi,” alisema mmoja wao.
No comments:
Post a Comment