WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania iko tayari kujifunza kutoka kwa
nchi nyingine ambazo ni wanachama wa Mpango wa Kujitathmni Kiutawala
Bora barani Afrika (APRM) ili iweze kuboresha hatua ilizofikia kwenye
mpango huo.
Ametoa
kauli hiyo jana jioni (Ijumaa, Agosti 26, 2016) wakati akichangia mada
katika Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Mpango wa Kujitathmni
Kiutawala Bora barani Afrika (APRM Forum) uliofanyika kwenye hoteli ya
InterContinental jijini Nairobi, Kenya.
“Nitumie
fursa hii kukiarifu kikao chako kwamba Tanzania imeshaanza kutekeleza
mpango kazi wa Kitaifa ambao umejikita kutatua changamoto katika sekta
za maji, elimu, kilimo, nishati na miundombinu kama zilivyoainishwa
kwenye kikao cha APRM,” alisema.
“Ili
kuhakikisha kuwa zinafanyiwa kazi haraka, changamoto hizi za kisekta
zimepewa kipaumbele kwenye Mpango wetu wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa
miaka mitano wa 2016-2021 ambao umejikita zaidi kwenye viwanda,”
aliongeza.
Tanzania
ilifanyiwa tathmini yake Januari, 2013 kwenye kikao cha Wakuu wa Nchi
za Umoja wa Afrika kilichofanyika Addis Ababa, Ethiopia.
Mapema,
akifungua mkutano huo, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisema viongozi wa
Afrika hawana budi kukubaliana na kuungana kutafuta suluhisho katika
ushindani wa kibiashara.
Alisema nchi wanachama wa mpango huo hawana budi kujenga umoja kama njia ya muafaka ya kufikia makubaliano hayo.
Wakati
huohuo, Rais Yoweri Museveni wa Uganda alisema bara la Afrika
linakabiliwa na changamoto 11 (strategic bottlenecks) ambazo
zinakwamisha maendeleo ya bara hilo na akataka zitafutiwe ufumbuzi ili
kuzisaidia nchi nyingi barani humo.
Akiwasilisha
mada binafsi katika mkutano huo, Rais Museveni alisema kwa zaidi ya
miaka 50, amekuwa kiongozi katika sehemu kadhaa na kwamba amebaini kuwa
changamoto hizo zimezuia ukuaji wa uchumi barani Afrika pamoja na
mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.
Alisema
asilimia kubwa ya changamoto hizo haikupata ufumbuzi hata wakati
malengo ya maendeleo ya milenia (MDGs) yalipokuwa yanatekelezwa.
Alizitaja
changamoto hizo kuwa ni mikanganyiko ya kiitikadi ambayo huzaa ubinafsi
na maslahi binafsi; kuwepo kwa mataifa dhaifu (weak states); nguvukazi
duni (kitaaluma na kiafya), uduni wa miundombinu (barabara, maji, umeme,
tehama) ambao unashindwa kuvutia uwekezaji; uhaba wa viwanda
unaolazimisha nchi kusafirisha mali ghafi na uhaba wa masoko ya bidhaa
zinazozalishwa barani Afrika.
Changamoto
nyingine ni uduni wa huduma za kijamii unaosababisha huduma mbovu
kwenye maeneo ya utalii, mabenki na mahoteli; kilimo duni kisichotumia
mbolea, dawa za kuua wadudu, mbegu za kisasa au njia za umwagiliaji;
makosa ya kisera kama vile ubinafishaji au utaifishaji mali
zinazomilikiwa na sekta binafsi; ukandamijazi wa demokrasia na ukosefu
wa maadili miongoni mwa watumishi wa umma.
Naye
Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini alisema kwa vile changamoto hizo
zinagusa nchi nyingi za Afrika, ni vema iundwe timu ya wataalamu
watakazipitia zote na kuainisha zipi zinafaa kufanyiwa kazi na kisha
taarifa yao iwasilishwe kwenye kikao kijacho cha Wakuu wa Nchi
wanachama.
Akifunga
mkutano huo, Rais Kenyatta aliitaka sekretarieti ya APRM ipitie
changaoto hizo na kuziwakilisha kwenye kikao chao kijacho ambacho
alisema kitafanyika Januari 2017, mjini Addis Ababa, Ethiopia katika
tarehe itakayopangwa baadaye.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, AGOSTI 27, 2016.
No comments:
Post a Comment