Showing posts with label SIASA. Show all posts
Showing posts with label SIASA. Show all posts

Thursday, September 1, 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Azindua Ripoti Ya Hali Ya Hewa Barani Africa


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Afrika wajiulize wanaweza kuchangia kitu gani katika kuboresha maisha ya mamilioni ya wakazi wa bara hilo.

Ametoa kauli hiyo Alhamisi, Agosti 31, 2016 usiku  wakati akizungumza na wawakilishi wa taasisi za kimataifa waliohudhuria uzinduzi wa taarifa ya Taasisi ya Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji barani Afrika (ICF) uliofanyika kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo alisema taasisi hiyo imesaidia kukuza uwekezaji kupitia miradi katika nchi mbalimbali za Afrika kwa kuimarisha mifumo ya ukusanyaji kodi, usajili wa biashara za wajasiriamali na upatikanaji wa leseni za biashara.

“Kutokana na kazi inayofanywa na taasisi hii, hali ya uwekezaji katika nchi nyingi imeimarika na bara la Afrika limekuwa mbia kwa wawekezaji kutokana na ushirikiano baina ya Serikali za nchi husika na sekta binafsi. Uchumi wa nyingi za Afrika umeimarika kuliko hapo awali,” alisema.

Akitoa mfano, Waziri Mkuu alisema zaidi ya wajasiriamali 500 kutoka Tanzania walipatiwa mafunzo kwa ushirikiano baina ya ICF, Serikali na ESAURP ili kuwajengea uwezo waweze kufanya biashara zao kwa tija zaidi. “Mafunzo hayo yaliwalenga wajasiriamali wadogo na wa kati ambao wanajihusisha na uvuvi, biashara za rejereja na jumla kutoka mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam”.

“Kupitia mafunzo hayo, wajasiriamali hao waliweza kusajili biashara, kurasimisha biashara zao, kuongeza mitaji na kujua namna ya kutunza taarifa za biashara zao,” alisema.

Mapema, Mwenyekiti Mwenza wa taasisi hiyo ambaye pia ni Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mhe. Benjamin Mkapa alisema kuna haja ya wananchi kubadili mitazamo yao juu ya sekta binafsi kwani nayo ni muhimu katika ujenzi wa uchumi kwa nchi yoyote ile.

“Watu wengi wanahisi kwamba wawekezaji ni wabaya. Hii si kweli. Tunapaswa kujenga mazingira ya kuwakubali kwa sababu wanakuja na mitaji yao na wao wanawakilisha michango kutoka kwa mamilioni ya wafanyakazi kutoka kwenye nchi zao. Hatupaswi kuwaona kwamba ni maadui,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Mstaafu wa Serikali ya awamu ya nne, Mhe. Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa kukubali kuiruhusu taasisi hiyo ya ICF iweke makao yake makuu hapa nchini wakati ilikuwa imeshakataliwa kufanya hivyo katika nchi nyingi ambako ilipeleka maombi yake.

Aliwataka viongozi mbalimbali watumie uzoefu uliowekezwa na taasisi hiyo kwenye uboreshaji wa mifumo ya mahakama na ukusanyaji kodi, utoaji wa leseni, urasmishaji wa biashara za wajasiriamali wadogo.

“Tunayo maeneo mengi ambayo tumefanya vizuri iwe ni katika TEHAMA, miundombinu, mahakama au mambo ya forodha. Uamuzi ni wenu juu ya jambo lipi muanze nalo katika kuboresha huduma ili kuharakisha maendeleo ya bara hili,” alisema.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

ALHAMISI, SEPTEMBA MOSI, 2016

Mapokezi ya Waziri Mkuu Mjini Dodoma Yaahirishwa Hadi Vikao vya Bunge Viishe



SERIKALI Mkoa wa Dodoma imesema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atahamia rasmi mkoani humo mara baada ya kumalizika kwa vikao vya Bunge vinavyoanza wiki ijayo, Septemba 6.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alisema baada ya kufika Dodoma, ataanza kuratibu utaratibu wa wizara mbalimbali kuhamia katika Makao Makuu hayo ya nchi.

Pamoja na hayo Jeshi la Polisi limejipanga kuongeza vituo vya Polisi ili kuimarisha ulinzi wakati serikali itakapohamia na hakuna mwananchi atakayenyang’anywa ardhi yake kwa sababu yoyote ile.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Rugimbana alisema kama mkoa walishauri ujio huo ufanyike mara baada ya kikao cha Bunge na Waziri Mkuu ameridhia suala hilo.

Alisema Waziri Mkuu atakuwa Mratibu wa wizara zote kuhamia Dodoma na kazi hiyo ataianza rasmi mara baada ya kuwasili mkoani humo.

Alisema maandalizi yanaendelea vizuri na ukarabati wa nyumba ya Waziri Mkuu umefikia asilimia 90.

Alisema Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christine Mndeme aliyekutana na makundi mbalimbali kwa ajili ya mapokezi ya Waziri Mkuu.

“Awali tulisema atakuja Septemba Mosi lakini baada ya kushauriana tumeona aje mara baada ya vikao vya Bunge kwani pilikapilika nyingi zitakuwa zimepungua, kama serikali ikiamua kuja leo tutaipokea kwani maandalizi ya serikali kuja Dodoma yamekamilika kwa asilimia 70,” alisema.

UVCCM yaivaa rasmi Chadema kwa kushindwa kufanya Maandamano ya UKUTA


Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), umewavaa viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kile walichodai kuendesha siasa za maigizo baada ya kushindwa kuzindua Operesheni UKUTA, Septemba 1.

Kupitia taaria yake kwa vyombo vya habari, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, amesema kuwa Chadema walijua kuwa hawana ubavu wa kufanya maandamano na mikutano nchi nzima Septemba 1 na kwamba walichofanya ni kuwatia hofu wananchi.

“UVCCM tulijua, tulielewa na kutambua bayana kwamba Chadema walikuwa wanafanya maigizo katika siasa, hawana ubavu wala jeuri ya kuandamana kwa madai ya kipuuzi na ambayo sio ya msingi kwa mustakabali wa nchi yetu,” alisema Shaka.

Aidha, Shaka alikanusha sababu zilizotolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuahirisha maandamano hayo kuwa wameombwa na viongozi wa dini ili waweze kukaa na pande zote kujaribu kutafuta suluhu kwa amani.

“UVCCM inatamka bayana kuwa hakuna majadiliano, mazungumzo wala mijadala itakayojadiliwa kati ya Serikali ya CCM na Chadema. Tunaomba Serikali ya Rais John Magufuli iendelee na mikakati yake ya kisera,” Shaka ameongeza.

Kaimu Katibu Mkuu huyo wa UVCCM alisisitiza kuwa Chadema hawana ubavu wa kufanya maandamano na mikuano nchi nzima Oktoba 1 kama walivyosema, baada ya kushindwa kufanya hivyo Septemba 1.

Shaka amesema wanachokifanya hivi sasa Chadema kinatokana na kushindwa kubuni mikakati ya kufanya siasa ili chama chao kiimarike na kukubarika.

Juzi, Chadema walitangaza kuahirisha uzinduzi wa oparesheni UKUTA nchi nzima, iliyokuwa imepangwa kufanyika jana (Septemba 1) kwa maandamano na mikutano nchi nzima.

UVCCM pia walitangaza kuahirisha maandamano yao ya nchi nzima waliyokuwa wamepanga kuyafanya Agosti 31 kwa lengo la kumpongeza Rais Magufuli kwa kazi aliyoifanya ndani ya kipindi kifupi.

Maandamano ya pande zote mbili yalipigwa marufuku na Jeshi la Polisi nchini.

Waziri Mwinyi: Mipaka ya Tanzania iko Salama.



Na: Lilian Lundo- Maelezo
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewahakikishia watanzania kwamba mipaka ya Tanzania ni salama.

Mhe. Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika kipindi cha Tunatekeleza kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC) alipokuwa akieleza mikakati ya wizara hiyo katika kuhakikisha mipaka ya Tanzania iko salama.

“Nchi iko salama, mipaka ya nchi iko shwari, ziko changamoto chache za nchi zinazotuzunguka kuwepo katika machafuko mfano Burundi hivyo wananchi wake kukimbilia Tanzania,” alifafanua Mhe. Dkt. Mwinyi.

Amesema Tanzania sio kisiwa, imejiunga na jumuiya mbali mbali kama Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Umoja wa Mataifa hivyo kupitia Jumuiya hizo Tanzania hupata maelekezo ya kuwapokea wakimbizi kutoka nchi zenye machafuko.

Hata hivyo Mhe. Dkt. Mwinyi amesema kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inahakikisha wakimbizi wanaoingia nchini wanafuata utaratibu unaotakiwa bila kuvunja sheria za nchi.

Pia ameeleza kuwa Tanzania inaendelea na mazungumzo ya amani na nchi ya Malawi juu ya mgogoro wa umiliki wa Ziwa Nyasa baina ya nchi hizo mbili ili kupata ufumbuzi wa amani, ambapo mazungumzo hayo ya yanaongozwa na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Benjamin William Mkapa.

Aidha, Mhe. Dkt. Mwinyi amesema kuwa kutokana na Wizara hiyo kufanya vizuri katika Ulinzi na Amani ya Nchi, Jumuiya ya Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Umoja wa Mataifa imeiomba nchi ya Tanzania kutoa Ulinzi wa  Amani kwa nchi za Sudani, Kongo na Lebanoni kutokana na machuko yanayoendelea katika nchi hizo.

Vile vile ameeleza kuwa, ushiriki wa Jeshi la Tanzania katika nchi zenye machafuko kunaisaidia Jeshi hilo kupata mafunzo ya kivita kutokana na Tanzania kuwa ni nchi ya amani hivyo kufanya baadhi ya wanajeshi kutoshiriki mafunzo ya uhalisia ya kivita tangu wanapoajiriwa mpaka kustaafu.

Saturday, August 27, 2016

Waziri Mkuu: Tanzania Iko Tayari Kujifunza Kutoka Nchi Nyingine



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania iko tayari kujifunza kutoka kwa nchi nyingine ambazo ni wanachama wa Mpango wa Kujitathmni Kiutawala Bora barani Afrika (APRM) ili iweze kuboresha hatua ilizofikia kwenye mpango huo.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Ijumaa, Agosti 26, 2016) wakati akichangia mada katika Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Mpango wa Kujitathmni Kiutawala Bora barani Afrika (APRM Forum) uliofanyika kwenye hoteli ya InterContinental jijini Nairobi, Kenya.

“Nitumie fursa hii kukiarifu kikao chako kwamba Tanzania imeshaanza kutekeleza mpango kazi wa Kitaifa ambao umejikita kutatua changamoto katika sekta za maji, elimu, kilimo, nishati na miundombinu kama zilivyoainishwa kwenye kikao cha APRM,” alisema.

“Ili kuhakikisha kuwa zinafanyiwa kazi haraka, changamoto hizi za kisekta zimepewa kipaumbele kwenye Mpango wetu wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano wa 2016-2021 ambao umejikita zaidi kwenye viwanda,” aliongeza.

Tanzania ilifanyiwa tathmini yake Januari, 2013 kwenye kikao cha Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika kilichofanyika Addis Ababa, Ethiopia.

Mapema, akifungua mkutano huo, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisema viongozi wa Afrika hawana budi kukubaliana na kuungana kutafuta suluhisho katika ushindani wa kibiashara.

Alisema nchi wanachama wa mpango huo hawana budi kujenga umoja kama njia ya muafaka ya kufikia makubaliano hayo.

Wakati huohuo, Rais Yoweri Museveni wa Uganda alisema bara la Afrika linakabiliwa na changamoto 11 (strategic bottlenecks) ambazo zinakwamisha maendeleo ya bara hilo na akataka zitafutiwe ufumbuzi ili kuzisaidia nchi nyingi barani humo. 

Akiwasilisha mada binafsi katika mkutano huo, Rais Museveni alisema kwa zaidi ya miaka 50, amekuwa kiongozi katika sehemu kadhaa na kwamba amebaini kuwa changamoto hizo zimezuia ukuaji wa uchumi barani Afrika pamoja na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.
 
Alisema asilimia kubwa ya changamoto hizo haikupata ufumbuzi hata wakati malengo ya maendeleo ya milenia (MDGs) yalipokuwa yanatekelezwa.

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni mikanganyiko ya kiitikadi ambayo huzaa ubinafsi na maslahi binafsi; kuwepo kwa mataifa dhaifu (weak states); nguvukazi duni (kitaaluma na kiafya), uduni wa miundombinu (barabara, maji, umeme, tehama) ambao unashindwa kuvutia uwekezaji; uhaba wa viwanda unaolazimisha nchi kusafirisha mali ghafi na uhaba wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa barani Afrika.

Changamoto nyingine ni uduni wa huduma za kijamii unaosababisha huduma mbovu kwenye maeneo ya utalii, mabenki na mahoteli; kilimo duni kisichotumia mbolea, dawa za kuua wadudu, mbegu za kisasa au njia za umwagiliaji; makosa ya kisera kama vile ubinafishaji au utaifishaji mali zinazomilikiwa na sekta binafsi; ukandamijazi wa demokrasia na ukosefu wa maadili miongoni mwa watumishi wa umma.

Naye Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini alisema kwa vile changamoto hizo zinagusa nchi nyingi za Afrika, ni vema iundwe timu ya wataalamu watakazipitia zote na kuainisha zipi zinafaa kufanyiwa kazi na kisha taarifa yao iwasilishwe kwenye kikao kijacho cha Wakuu wa Nchi wanachama.

Akifunga mkutano huo, Rais Kenyatta aliitaka sekretarieti ya APRM ipitie changaoto hizo na kuziwakilisha kwenye kikao chao kijacho ambacho alisema kitafanyika Januari 2017, mjini Addis Ababa, Ethiopia katika tarehe itakayopangwa baadaye. 
 
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, AGOSTI 27, 2016.