Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita imemtoza faini ya Sh800,000
mwalimu wa Shule ya Sekondari Msalala, Henry Tagata kwa kuisababishia
Serikali hasara ya zaidi ya Sh9 milioni kwa kupokea mishahara akiwa
hayupo kwenye kituo chake cha kazi.
Mshtakiwa huyo alilipa kiasi hicho cha fedha na kunusurika kutumikia
kifungo cha miaka mwili jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa hilo.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama
hiyo, Ushindi Swalo alisema ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na
waendesha mashtaka wa Takukuru juzi, Kelvin Mrusuri na Agustino Mtaki
umethibitisha pasipo shaka kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.
Ilidaiwa mahakamani hapo na Mrusuri kuwa Agosti, 2010 hadi Aprili,
2014, mshtakiwa akiwa mwalimu wa shule hiyo alitoweka kwenye kituo chake
cha kazi na kuendelea kupokea mshahara na kuisababishia Serikali hasara
ya zaidi ya fedha hizo.
Aliendelea kudai kuwa mshtakiwa huyo akiwa ni mtumishi hewa,
aliisababishia Serikali hasara kinyume na aya ya 10(1) jedwali la kwanza
na vifungu vya 57(1) na 60 (2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi kwa kupokea
malipo ya mshahara asiyo stahili kwa kipindi ambacho hayuko kazini.
Katika shauri hilo namba sita ya mwaka 2016 la uhujumu uchumi,
mshtakiwa alitakiwa kurejesha fedha za Serikali alizopokea kama mshahara
akiwa hayuko kazini.
Hakimu Swalo alidai mahakamani hapo kuwa ametoa adhabu ya kifungo cha
miaka miwili au kulipa faini ya Sh800,00 ili iwe fundisho kwa watumishi
wengine wenye tabia kama ya mshtakiwa huyo.
Mshtakiwa huyo alilipa faini hiyo na kuachiwa huru.
No comments:
Post a Comment