WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Afrika wajiulize wanaweza
kuchangia kitu gani katika kuboresha maisha ya mamilioni ya wakazi wa
bara hilo.
Ametoa kauli hiyo Alhamisi, Agosti 31, 2016 usiku wakati akizungumza na wawakilishi wa taasisi za kimataifa waliohudhuria uzinduzi wa taarifa ya Taasisi ya Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji barani Afrika (ICF) uliofanyika kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Waziri
Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo alisema taasisi
hiyo imesaidia kukuza uwekezaji kupitia miradi katika nchi mbalimbali za
Afrika kwa kuimarisha mifumo ya ukusanyaji kodi, usajili wa biashara za
wajasiriamali na upatikanaji wa leseni za biashara.
“Kutokana
na kazi inayofanywa na taasisi hii, hali ya uwekezaji katika nchi
nyingi imeimarika na bara la Afrika limekuwa mbia kwa wawekezaji
kutokana na ushirikiano baina ya Serikali za nchi husika na sekta
binafsi. Uchumi wa nyingi za Afrika umeimarika kuliko hapo awali,”
alisema.
Akitoa
mfano, Waziri Mkuu alisema zaidi ya wajasiriamali 500 kutoka Tanzania
walipatiwa mafunzo kwa ushirikiano baina ya ICF, Serikali na ESAURP ili
kuwajengea uwezo waweze kufanya biashara zao kwa tija zaidi. “Mafunzo
hayo yaliwalenga wajasiriamali wadogo na wa kati ambao wanajihusisha na
uvuvi, biashara za rejereja na jumla kutoka mikoa ya Mwanza na Dar es
Salaam”.
“Kupitia
mafunzo hayo, wajasiriamali hao waliweza kusajili biashara, kurasimisha
biashara zao, kuongeza mitaji na kujua namna ya kutunza taarifa za
biashara zao,” alisema.
Mapema,
Mwenyekiti Mwenza wa taasisi hiyo ambaye pia ni Rais Mstaafu wa awamu
ya tatu, Mhe. Benjamin Mkapa alisema kuna haja ya wananchi kubadili
mitazamo yao juu ya sekta binafsi kwani nayo ni muhimu katika ujenzi wa
uchumi kwa nchi yoyote ile.
“Watu
wengi wanahisi kwamba wawekezaji ni wabaya. Hii si kweli. Tunapaswa
kujenga mazingira ya kuwakubali kwa sababu wanakuja na mitaji yao na wao
wanawakilisha michango kutoka kwa mamilioni ya wafanyakazi kutoka
kwenye nchi zao. Hatupaswi kuwaona kwamba ni maadui,” alisema.
Alitumia
fursa hiyo kumshukuru Rais Mstaafu wa Serikali ya awamu ya nne, Mhe.
Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa kukubali kuiruhusu taasisi hiyo ya ICF
iweke makao yake makuu hapa nchini wakati ilikuwa imeshakataliwa
kufanya hivyo katika nchi nyingi ambako ilipeleka maombi yake.
Aliwataka
viongozi mbalimbali watumie uzoefu uliowekezwa na taasisi hiyo kwenye
uboreshaji wa mifumo ya mahakama na ukusanyaji kodi, utoaji wa leseni,
urasmishaji wa biashara za wajasiriamali wadogo.
“Tunayo
maeneo mengi ambayo tumefanya vizuri iwe ni katika TEHAMA, miundombinu,
mahakama au mambo ya forodha. Uamuzi ni wenu juu ya jambo lipi muanze
nalo katika kuboresha huduma ili kuharakisha maendeleo ya bara hili,”
alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, SEPTEMBA MOSI, 2016
No comments:
Post a Comment