Katika dunia ya leo mawasiliano ni kitu muhimu sana katika maisha yetu. Mawasiliano ndio yanatuwezesha mimi na wewe kuweza kuwasiliana na kupashana habari katika makala hii. Huwezi kupata huduma yoyote bila mawasiliano. Mawasiliano bora ndio yanamuwezesha mtu kupata kazi au huduma nzuri kwa urahisi. Makampuni ya simu yanatumia lugha ya ushawishi ili kuweza kukuvuta wewe kama wangetumia lugha mbaya yaani mawasiliano mabovu wasingeweza kukushawishi.
Mawasiliano mazuri na watu ndio yanakupa au kukuhakikishia kupata fursa nzuri kwa watu. Watu wanashindwa kufanikiwa katika mambo mengi ni kwa sababu tu ya kutokuwa na mawasiliano mazuri na kukosa lugha ya ushawishi. Unaweza kuwa na kitu kizuri lakini jinsi unavyokiwasilisha kwa lugha ya hovyo nao watu watakuchukulia siyo mtu makini. Mafanikio tunayoyatafuta yanapatikana kwa watu hivyo ni lazima uwe na mawasiliano mazuri na mahusiano mazuri na watu. Pia inabidi kutumia mawasiliano sahihi kulingana na sehemu na mtu au watu husika. Unapokuwa unawasiliana na watu tumia lugha rasmi na siyo lugha ya mtaani kwani lugha rasmi inakutambulisha kuwa wewe ni mtu makini na watu watakuheshimu na kujenga imani na wewe.
Epuka mawasiliano yanayoweza kuwagawa watu kulingana na itikadi za kiimani tumia mawasiliano bora ambayo yanaweza kutumika kwa mtu yoyote yule bila kumgawa kinamna yoyote ile. Na tofautisha watu, mtu, kundi, taasisi, kampuni, rafiki, mpenzi katika mawasiliano.
Mawasiliano katika biashara; katika biashara mawasiliano bora na huduma bora ndio yanayoweza kumshawishi mteja wako. Mteja anahitaji lugha nzuri ya ushawishi na siyo kumlazimisha. Lugha mbaya ni kero na inaweza kusababisha kumpoteza mteja. Kama mfanyabiashara tumia lugha nzuri ya ushawishi itakayomvutia mteja wako hata kama alikuwa hana mpango wa kununua atanunua tu kulingana na lugha nzuri ya ushawishi na ukarimu wa mtoa huduma.
Katika biashara epuka tabia ya kumsalimia mtu kwa lugha isiyo rasmi acha mazoea kabisa ukimsalimia mtu katika lugha ya mtaani yaani lugha isiyo rasmi atakuoana na wewe siyo mtu makini katika kazi yako. Katika salamu msalimu mtu habari yako ndugu, habari ya kazi nk. Ile salamu rasmi na siyo unakwenda kuwasilisha biashara yako unawasalimu watu niaje, shwari nk. Lugha hizi siyo rasmi zinakufanya uonekane siyo makini. Kwa hiyo katika biashara tumia lugha rasmi yeye ushawishi na siyo lugha ya mtaani.
Kama unajua jina la mteja wako basi muite jina lake kwani mtu anafarijika sana anapoitwa jina lake halisi na tena kwa ufasaha. Muite mtu jina lile analopenda kama anapenda umuite jina analopenda muite. Epuka kukatisha jina la mtu kama unaweza kumuita jina zima muite atafarijika zaidi. Usisahau kusema asante kwa mteja na kama unawasiliana naye kwa email, simu nk usitumie vifupi utaonekana hauko makini na hujakua kwa mfano unaandika xaxa badala ya sasa huo ni utoto waachie watu ambao wako katika hatua ya ukuaji na siyo wewe. Vivyo hivyo, tumia lugha rasmi katika maswala ya kiofisi.
Katika mahusiano; tofautisha unawasiliana na nani; mpenzi wako, rafiki yako, ndugu, jamaa na marafiki. Katika mahusiano ya kimapenzi epuka kitu kinachoitwa mazoea kwani watu waliokuwa katika mahusiano ya kimapenzi kama mke na mume huwa wanajisahau sana katika mawasiliano. Unapomtumia mwenza wako ujumbe lazima utofautishe na ujumbe unaomtumia rafiki yako. Watu wanaua mahusiano yao kwa kukosa mawasiliano mazuri mfano mtu anamtumia mpenzi wake ujumbe kama vile anamtumia rafiki bila hata kuweka vionjo mbalimbali vya kimahaba vitakavyompa faraja na upendo. Unapomtumia jumbe zilizokosa vionjo akipata mtu anayemwekea vionjo katika jumbe itakuletea dosari katika mahusiano yako kama mwenzako ameweza kuweka vionjo kwa kutumia muda wake na wewe unamtumia ujumbe mkavu kwani utapungukiwa nini ukituma kama yeye alivyotuma. Kwa hiyo, ni vema kuepuka mazoea katika mawasiliano kwani mazoea katika mawasiliano ndiyo yanavunja mahusiano.
Mahusiano ya kirafiki; unapomsalimu rafiki ni vizuri zaidi kumwita jina lake na mwisho wa mawasiliano sema asante au kama ni ujumbe wa kimaandishi andika asante mwishoni mwa jumbe yako kwa kufanya hivyo unakuwa unathamini muda wake kwa kusoma ujumbe wako, epuka vifupi vya kijinga kwani vifupi vimekuwa ni kero kwa sasa mtu anakuandikia xalamu badala ya salamu, xaxa badala ya sasa ukimuona mtu anakuandikia hivi ujue bado hajakua yuko katika hatua za ukuaji. Mtu makini hawezi kuandika vifupi. Pendelea kutumia lugha ya mawasiliano iliyo rasmi kwani itakusaidia kuonekana mtu makini katika mambo yako kuliko lugha za mtaani.
Mawasiliano lazima yawe na mrejesho yaani feedback, sasa mtu anapokusalimu kwa njia yoyote ile ya kupasa umpe mrejesho na siyo kukaa kimya tu. Mawasiliano yoyote yana gharama kuna gharama za muda, pesa, nguvu nk, hivyo mtu anapokusalimu ujue ametumia gharama hivyo basi unapaswa kuthamini salamu au mawasiliano. Mawasiliano mazuri ni yale yenye mrejesho. Kuna maneno muhimu sana katika mawasiliano kama vile samahani, asante, naomba na nk. Neno asante ni neno dogo lakini lina maana au uzito mkubwa sana linampa mtu hamasa juu ya kitu fulani. Sema asante mtu anapokupatia kitu siyo kukaa kimya.
Kwa hiyo, mawasiliano ni kitu muhimu sana, maisha ni mawasiliano ya kila siku kwani mahitaji yetu mengi ya kila siku tunayapata kwa njia ya mawasiliano. Kuna watu wanakosa kazi kwa sababu ya lugha mbaya au mawasiliano mfano mtu anapoenda katika usaili anatakiwa kutumia lugha rasmi na mawasiliano mazuri ili aweze kuwashawishi na kupata ajira. Mwingine anakwenda katika ofisi za watu na kuwasalimia watu kihuni au anakwenda mbele ya kadamnasi anawasalimu watu kihuni mfano oya niaje salamu kama hizi ni kero kwa watu na katika kundi la watu ujue kuna watu wa aina mbalimbali hivyo ni lazima utambue itifaki za watu na kuzizingatia. Hivyo unaweza kuwa na shida ukakosa kusaidiwa na watu kukupuuza kulingana na lugha au mawasiliano mabovu uliyotumia.
Mwisho, tumia mbinu bora za mawasiliano ili kujenga mahusiano bora na watu waliokuzunguka. Kama mtu anawasiliana na wewe kwa lugha ya Kiswahili usimjibu kwa kingereza.
No comments:
Post a Comment