Anachozungumzia bwana M ni kuwa mitandao ya kijamii kama WhatsApp , Facebook , na Instagram inawapa watu wengi uwezo wa kujielezea yale ambayo pengine katika mazingira waliyopo wanashindwa kujieleza.
Athari za Uhuru wa kujieleza ndani ya WhatsApp, Facebook , Instagram
Hata hivyo hapo katika kujielezea ndipo kunapoweza leta matatizo badala ya kumsaidia mtumiaji wa mtandao. Nazungumzia pale ambapo mtu badala ya kukaa chini na mhusika na kumueleza malalamiko yako, wewe unatoka na kuenda kutangaza matatizo yako au kutoridhika kwako au hasira zako huko mtandaoni.
Status/Posts za WhatsApp, Facebook, Instagram zinasema mengi
Kuna watu unaweza jua mood zao kupitia status wanazoweka. Kwa yule ambayo amekukosea au mliye katika mfarakano, yeye hatojisikia vizuri hata kidogo, na huko unapoenda kutangaza wala hakuna wa kukusaidia.
Tafsiri ya posts zako za WhatsApp, Facebook, Instagram
Jambo lingine la kukumbuka ni kuwa kama unapopost malalamiko, kashfa au kejeli kwa kuwa umekasirishwa au unahisi kuonewa na mtu fulani , unajijengea picha mbaya kwa baadhi ya watu kuwa wewe si mzuri katika mahusiano ya mtu na mtu, hivyo watu wakae mbali nawe , kwani hujui namna ya kumaliza matatizo kati yako na watu unaohusiana nao, badala yake unakimbilia mtandaoni.
Athari zake
Unapojionyesha kuwa hauna uwezo wa kumaliza matatizo yako bila kuenda mtandaoni , unajiweka katika mazingira magumu mfano ya kupata kazi, au kupata washirika wa kufanya nao dili za biashara n.k kwakuwa wataogopa kuaibishwa mtandaoni.
Pia kujizoesha kukimbilia mtandaoni kutangaza matatizo yako badala ya kutafuta njia ya kuyamaliza huko pembeni , kunadhoofisha uwezo wako wa kujenga mahusiano bora.
Hitimisho
Pamoja na umuhimu wa mitandao ya jamii ya kutuweka karibu na watu wengi, tusisahau kujenga mahusiano ya mtu mmoja mmoja. Na lolote linalotokea baina yako na mtu au kundi fulani huko nje ya mitandao ya kijamii, jitahidi ulimalize huko huko nje, na sio kulipeleka mtandaoni kana kwamba huko mtandaoni kuna majaji wa kukupatia haki.