SERIKALI
imesema itaanza kutumia mbinu mpya kuwadhibiti madaktari na wauguzi
wanaoiba dawa za serikali na kisha kuziuza kwenye maduka ya watu
binafsi.
Tamko hilo lilitolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Mhandisi John Kijazi alipoenda kukabidhi magodoro 50 katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dar es Salaam Mwananyala yaliyotolewa na umoja wa makanisa ya Kipentekoste nchini.
Kijazi
alisema mbinu hiyo itasaidia kuwabaini kiurahisi watumishi hao kwani
itaendeshwa kwa siri ambapo kila kitengo katika wizara ya afya kutakuwa
na mwakilishi atakayesaidia kutoa taarifa pindi atakapoona jambo hilo.
“Mimi
niwatake wenye tamaa waache mara moja haiwezekani dawa serikali inunue
kwaajili ya kuwapatia wananchi bure mtu mmoja kwa manufaa yake azipeleke
kwa wafanyabiasha kuuza wananchi wakose dawa na kuanza kuhangaika”alisema Kijazi.
Pia
amewataka wauguzi kuhakikisha kwamba malalamiko yanayotolewa na
wananchi yanafanyiwa kazi mara moja na kuongeza serikali haitasita
kumchukulia hatua mtu yeyote atakayebainika kumnyanyasa mgonjwa.
Alisema
wagonjwa wamekuwa wakitoa malalamiko mengi juu ya huduma zinazotolewa
katika hospitali ya Mwananyamala hivyo amewataka watendaji kubadilika
ili kuepuka malalamiko yasiyo ya msingi.
Alisema
ni lazima watoa huduma za afya wakazingatia nidhamu na weledi katika
utendaji wa kazi kwani hawakulazimishwa kusomea taaluma hiyo na kuongeza
kuwa fani zipo nyingi hivyo ambaye anaona hawezi kufanya yanayotakiwa
aachie wengine.
Pamoja
na hayo amezitaka hospitali zote kuanzisha dawati la malalamiko ili
wanaohudumiwa wapate pakusemea pindi wanapofanyiwa vitendo vya
unyanyasaji ikiwa ni pamoja na kucheleweshewa huduma au kuombwa fedha
ili kuwahishiwa huduma ili hali ikiwa ni haki yao.
Hata hivyo ametaka madawati hayo kuwa wazi masaa 24 ili wananchi wapate muda mwingi wakujieleza na sio kusubiri kuelezea hisia zao pale wanapoona viongozi wakitembelea vituo hivyo.
Kijazi alitembelea wodi
mbalimbali hospitalini hapo ikiwamo wodi ya wazazi, Wanaume, Watoto,
Wanawake na watoto njiti ambapo alipata kujionea baadhi ya wagonjwa
wakilala zaidi ya mmoja kwenye kitanda kimoja kutokana na kukosekana kwa
vitanda.
Naye
Mganga mkuu msaidizi katika hospitali hiyo Delila Moshi alieleza
matatizo yanayoikabili hospitali hiyo kuwa ni pamoja na madeni ambapo
inadaiwa stahiki za watumishi Sh. milioni 500 ambazo ni fedha za likizo
kwa wafanyakazi, Sare za kazi, Nyumba na posho za masaa ya ziada.
Moshi
alisema hospitali hiyo pia ina ukosefu wa vifaa vya kisasa kama CT Scan
hali inayosababisha wagonjwa kupewa rufaa ya kwenda muhimbili kwaajili
ya vipimo zaidi, Ukosefu wa chumba cha uangalizi wa wagonjwa mahututi
(ICU) na Daktari bingwa wa mifupa na wagonjwa wa dharura.
Tatizo
lingine ni wingi wa wagonjwa wa msamaha ambapo kwa kuanzia januari hadi
desemba mwaka jana zaidi ya bilioni 2 zilitumika huku kwa mwezi wakitoa
matibabu ya zaidi ya milioni 100 bure.
No comments:
Post a Comment