Saturday, September 24, 2016

ZIFAHAMU ATHARI HIZI ZA WHATSAPP, FACEBOOK, INSTAGRAM KATIKA MAHUSIANO


Faida za WhatsApp , Facebook,  Instagram au mitandao mingine ya kijamii unazijua ? Au kufupisha habari je, wewe unanufaika na hii mitandao ya kijamii ?  Kutana na bwana M, ambaye anadai kwake faida kubwa ya mitandao hii ni kuwa inamfanya asijione mpweke.  Ni sehemu  ya burudani na kufahamu nini kinaendelea katika ulimwengu unaomzunguka.

Anachozungumzia bwana M ni kuwa mitandao  ya kijamii kama WhatsApp , Facebook , na Instagram inawapa watu wengi uwezo wa kujielezea yale ambayo pengine katika mazingira waliyopo wanashindwa kujieleza.

Athari za Uhuru wa kujieleza ndani ya WhatsApp, Facebook , Instagram
Hata hivyo hapo katika kujielezea ndipo kunapoweza leta matatizo badala ya kumsaidia mtumiaji wa mtandao. Nazungumzia pale ambapo mtu badala ya kukaa chini na mhusika na kumueleza malalamiko yako, wewe unatoka na kuenda kutangaza matatizo yako au kutoridhika kwako au hasira zako huko mtandaoni.

Status/Posts za WhatsApp, Facebook, Instagram zinasema mengi
Kuna watu unaweza jua mood zao kupitia status wanazoweka. Kwa yule ambayo amekukosea au mliye katika mfarakano, yeye hatojisikia vizuri hata kidogo, na huko unapoenda kutangaza wala hakuna wa kukusaidia.

Tafsiri ya posts zako za WhatsApp, Facebook, Instagram
Jambo lingine la kukumbuka ni kuwa kama unapopost malalamiko, kashfa au kejeli kwa kuwa umekasirishwa au unahisi kuonewa na mtu fulani , unajijengea picha mbaya kwa baadhi ya watu kuwa wewe si mzuri katika mahusiano ya mtu na mtu, hivyo watu wakae mbali nawe , kwani hujui namna ya kumaliza matatizo kati yako na watu unaohusiana nao, badala yake unakimbilia mtandaoni.
Athari zake

Unapojionyesha kuwa hauna uwezo wa kumaliza matatizo yako bila kuenda mtandaoni , unajiweka katika mazingira magumu mfano ya kupata kazi, au kupata washirika wa kufanya nao dili za biashara n.k kwakuwa wataogopa kuaibishwa mtandaoni.

Pia kujizoesha kukimbilia mtandaoni kutangaza matatizo yako badala ya kutafuta njia ya kuyamaliza huko pembeni , kunadhoofisha uwezo wako wa kujenga mahusiano bora.
Hitimisho

Pamoja na umuhimu wa mitandao ya jamii ya kutuweka karibu na watu wengi, tusisahau kujenga mahusiano ya mtu mmoja mmoja. Na lolote linalotokea baina yako na mtu au kundi fulani huko nje ya mitandao ya kijamii, jitahidi ulimalize huko huko nje, na sio kulipeleka mtandaoni kana kwamba huko mtandaoni kuna majaji wa kukupatia haki.

Monday, September 19, 2016

ORODHA YA MAJINA YA WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA NA KIDATO CHA TANO NA VYUO VYA UFUNDI KWA MWAKA 2016

Tumia namba ya shule, jina la mwanafunzi au shule atokayo kurahisisha kupata shule aliyochaguliwa mwanafunzi

1

Tuesday, September 13, 2016

UTAJUAJE KAMA UNA UPUNGUFU WA MAJI MWILINI?


Umeshawahi kwenda hospitali kumlalamikia daktari kuwa mwili wako hauna nguvu na unajisikia kuchokachoka sana na baada ya kukuchunguza, akakwambia huna tatizo lolote isipokuwa una upungufu wa maji mwilini tu?

Mwili kuishiwa nguvu huwa ni miongoni mwa dalili za upungufu wa maji mwilini na chanzo kikiwa ni wewe mwenyewe kutopenda kunywa maji. Ni kawaida kwa baadhi ya watu kutokunywa maji hadi pale wanaposikia kiu.

Katika makala ya leo, nitakujuza dalili za mwili kuishiwa maji ambazo hujitokeza na kukuhimiza kunywa maji hata kabla hujasikia kiu. Uonapo dalili hizo, hupaswi kuzipuuzia bali kunywa maji kwa wingi tena haraka.

UPUNGUFU WA MAJI MWILINI NI NINI?
Pale mwili unapopoteza kiasi kingi cha maji kwa njia mbalimbali, ikiwemo jasho na mkojo, mwili hupungukiwa maji na hivyo mtu huyo huambiwa ana upungufu wa maji. Tunaelezwa kuwa karibu theluthi mbili ya miili yetu imejaa maji.

Ili mwili uweze kufanya kazi yake vizuri, kiwango cha maji mwilini hakipaswi kupungua hata kidogo, hivyo kila mtu ana wajibu wa kunywa maji ya kutosha kila siku ili kulinda kiwago chake cha maji kisipungue na kinapopungua ndipo hapo mwili huanza kuonesha dalili za kukaukiwa maji (dehydration).

NINI HUSABABISHA?
Sababu zinazosabababisha mwili kukaukiwa maji huweza kuwa nyingi, lakini zinazojulikana zaidi ni pamoja na:
Kuacha kunywa maji
Kukaa kwenye joto kwa muda mrefu
Kunywa kiwango kikubwa cha pombe,
Ungonjwa wa kisukari ambao husababisha mtu kukojoa mara kwa mara
Kutokwa na jasho jingi, kwa sababu ya ama kufanya kazi ngumu au mazoezi. Hivyo inashauriwa mtu anayetokwa jasho jingi kunywa maji mara kwa mara wakati akiendelea na shughuli inayomtoa jasho.
Kama ukiugua au ukipatwa na homa kali, huweza kupungukiwa na maji mwilini
Kutapika na kuharisha nako huweza kupoteza maji mwilini.

DALILI ZA KUKAUKIWA MAJI KWA WATOTO
Kwa kawaida, dalili za upungufu wa maji mwilini hujitokeza zaidi kwa watoto wadogo kuliko watu wazima au wazee. Dalili za upungufu wa maji mwilini kwa watoto huweza kusabababishwa ama na kuharisha, kutapika, kutokunywa maji au vimiminika vingine vya kutosha.
Mtoto mwenye dalili za upungufu wa maji huweza kuonesha dalili zifutazo:

Kukojoa mara chache sana
Mtoto kutokuwa mchangamfu
Macho, tumbo au mashavu kubonyea
Mdomo na ulimi kukauka
Mtoto kulia mara kwa mara na anapolia machozi hayatoki.

DALILI ZA UPUNGUFU WA MAJI KWA WAZEE
Dalili za upungufu wa maji kwa wazee ni tofauti na watu wazima. Wazee wa umri zaidi ya miaka 60 huwa na ngozi iliyosinyaa na hata ukiiminya, hubaki katika hali hiyo kwa muda na unapoikwaruza alama hubaki.

Halikadhalika, wazee hukosa haja ndogo kwa muda mrefu, hupungukiwa uzito kwa kiasi kikubwa na hupatwa na homa.

DALILI ZA UPUNGUFU WA MAJI KWA WAJA WAZITO
Upungufu wa maji mwilini kwa waja wazito ni hatari kwa mama pamoja na mtoto. Dalili zinazoweza kujitokeza kwa waja wazito ni pamoja na:

Kukojoa mkojo wa njano nyeusi
Kuumwa na kichwa
Mwili kukosa nguvu
Kichefuchefu na kutapika
Kukaukwa na mdomo

Ili kujiepusha na matatizo ya upungufu wa maji na hatimaye kujikuta unakumbwa na dalili kadhaa zilizoelezewa hapo, ambazo ziko pia kwa watu wazima wengine, ni kuwa na mazoea ya kunywa maji ya kutosha kila siku. Hata utakapozidiwa na kukimbizwa hospitali, hakuna dawa nyingine utakayopewa zaidi ya maji (re-hydrating solution). Kwa nini usubiri hali hiyo ikutokee wakati unaweza kuizuia kwa kunywa maji tu

Umuhimu Wa Mawasiliano Katika Kujenga Mahusiano Bora Ya Kijami


Habari rafiki na mpenzi msomaji wa Amka Mtanzania? Natumaini unaendelea vema katika kuboresha maisha yako na karibu katika makala yetu ya leo.

Katika dunia ya leo mawasiliano ni kitu muhimu sana katika maisha yetu. Mawasiliano ndio yanatuwezesha mimi na wewe kuweza kuwasiliana na kupashana habari katika makala hii. Huwezi kupata huduma yoyote bila mawasiliano. Mawasiliano bora ndio yanamuwezesha mtu kupata kazi au huduma nzuri kwa urahisi. Makampuni ya simu yanatumia lugha ya ushawishi ili kuweza kukuvuta wewe kama wangetumia lugha mbaya yaani mawasiliano mabovu wasingeweza kukushawishi.

Mawasiliano mazuri na watu ndio yanakupa au kukuhakikishia kupata fursa nzuri kwa watu. Watu wanashindwa kufanikiwa katika mambo mengi ni kwa sababu tu ya kutokuwa na mawasiliano mazuri na kukosa lugha ya ushawishi. Unaweza kuwa na kitu kizuri lakini jinsi unavyokiwasilisha kwa lugha ya hovyo nao watu watakuchukulia siyo mtu makini. Mafanikio tunayoyatafuta yanapatikana kwa watu hivyo ni lazima uwe na mawasiliano mazuri na mahusiano mazuri na watu. Pia inabidi kutumia mawasiliano sahihi kulingana na sehemu na mtu au watu husika. Unapokuwa unawasiliana na watu tumia lugha rasmi na siyo lugha ya mtaani kwani lugha rasmi inakutambulisha kuwa wewe ni mtu makini na watu watakuheshimu na kujenga imani na wewe.

Epuka mawasiliano yanayoweza kuwagawa watu kulingana na itikadi za kiimani tumia mawasiliano bora ambayo yanaweza kutumika kwa mtu yoyote yule bila kumgawa kinamna yoyote ile. Na tofautisha watu, mtu, kundi, taasisi, kampuni, rafiki, mpenzi katika mawasiliano.

Mawasiliano katika biashara; katika biashara mawasiliano bora na huduma bora ndio yanayoweza kumshawishi mteja wako. Mteja anahitaji lugha nzuri ya ushawishi na siyo kumlazimisha. Lugha mbaya ni kero na inaweza kusababisha kumpoteza mteja. Kama mfanyabiashara tumia lugha nzuri ya ushawishi itakayomvutia mteja wako hata kama alikuwa hana mpango wa kununua atanunua tu kulingana na lugha nzuri ya ushawishi na ukarimu wa mtoa huduma.
Katika biashara epuka tabia ya kumsalimia mtu kwa lugha isiyo rasmi acha mazoea kabisa ukimsalimia mtu katika lugha ya mtaani yaani lugha isiyo rasmi atakuoana na wewe siyo mtu makini katika kazi yako. Katika salamu msalimu mtu habari yako ndugu, habari ya kazi nk. Ile salamu rasmi na siyo unakwenda kuwasilisha biashara yako unawasalimu watu niaje, shwari nk. Lugha hizi siyo rasmi zinakufanya uonekane siyo makini. Kwa hiyo katika biashara tumia lugha rasmi yeye ushawishi na siyo lugha ya mtaani.

Kama unajua jina la mteja wako basi muite jina lake kwani mtu anafarijika sana anapoitwa jina lake halisi na tena kwa ufasaha. Muite mtu jina lile analopenda kama anapenda umuite jina analopenda muite. Epuka kukatisha jina la mtu kama unaweza kumuita jina zima muite atafarijika zaidi. Usisahau kusema asante kwa mteja na kama unawasiliana naye kwa email, simu nk usitumie vifupi utaonekana hauko makini na hujakua kwa mfano unaandika xaxa badala ya sasa huo ni utoto waachie watu ambao wako katika hatua ya ukuaji na siyo wewe. Vivyo hivyo, tumia lugha rasmi katika maswala ya kiofisi.

Katika mahusiano; tofautisha unawasiliana na nani; mpenzi wako, rafiki yako, ndugu, jamaa na marafiki. Katika mahusiano ya kimapenzi epuka kitu kinachoitwa mazoea kwani watu waliokuwa katika mahusiano ya kimapenzi kama mke na mume huwa wanajisahau sana katika mawasiliano. Unapomtumia mwenza wako ujumbe lazima utofautishe na ujumbe unaomtumia rafiki yako. Watu wanaua mahusiano yao kwa kukosa mawasiliano mazuri mfano mtu anamtumia mpenzi wake ujumbe kama vile anamtumia rafiki bila hata kuweka vionjo mbalimbali vya kimahaba vitakavyompa faraja na upendo. Unapomtumia jumbe zilizokosa vionjo akipata mtu anayemwekea vionjo katika jumbe itakuletea dosari katika mahusiano yako kama mwenzako ameweza kuweka vionjo kwa kutumia muda wake na wewe unamtumia ujumbe mkavu kwani utapungukiwa nini ukituma kama yeye alivyotuma. Kwa hiyo, ni vema kuepuka mazoea katika mawasiliano kwani mazoea katika mawasiliano ndiyo yanavunja mahusiano.

Mahusiano ya kirafiki; unapomsalimu rafiki ni vizuri zaidi kumwita jina lake na mwisho wa mawasiliano sema asante au kama ni ujumbe wa kimaandishi andika asante mwishoni mwa jumbe yako kwa kufanya hivyo unakuwa unathamini muda wake kwa kusoma ujumbe wako, epuka vifupi vya kijinga kwani vifupi vimekuwa ni kero kwa sasa mtu anakuandikia xalamu badala ya salamu, xaxa badala ya sasa ukimuona mtu anakuandikia hivi ujue bado hajakua yuko katika hatua za ukuaji. Mtu makini hawezi kuandika vifupi. Pendelea kutumia lugha ya mawasiliano iliyo rasmi kwani itakusaidia kuonekana mtu makini katika mambo yako kuliko lugha za mtaani.

Mawasiliano lazima yawe na mrejesho yaani feedback, sasa mtu anapokusalimu kwa njia yoyote ile ya kupasa umpe mrejesho na siyo kukaa kimya tu. Mawasiliano yoyote yana gharama kuna gharama za muda, pesa, nguvu nk, hivyo mtu anapokusalimu ujue ametumia gharama hivyo basi unapaswa kuthamini salamu au mawasiliano. Mawasiliano mazuri ni yale yenye mrejesho. Kuna maneno muhimu sana katika mawasiliano kama vile samahani, asante, naomba na nk. Neno asante ni neno dogo lakini lina maana au uzito mkubwa sana linampa mtu hamasa juu ya kitu fulani. Sema asante mtu anapokupatia kitu siyo kukaa kimya.

Kwa hiyo, mawasiliano ni kitu muhimu sana, maisha ni mawasiliano ya kila siku kwani mahitaji yetu mengi ya kila siku tunayapata kwa njia ya mawasiliano. Kuna watu wanakosa kazi kwa sababu ya lugha mbaya au mawasiliano mfano mtu anapoenda katika usaili anatakiwa kutumia lugha rasmi na mawasiliano mazuri ili aweze kuwashawishi na kupata ajira. Mwingine anakwenda katika ofisi za watu na kuwasalimia watu kihuni au anakwenda mbele ya kadamnasi anawasalimu watu kihuni mfano oya niaje salamu kama hizi ni kero kwa watu na katika kundi la watu ujue kuna watu wa aina mbalimbali hivyo ni lazima utambue itifaki za watu na kuzizingatia. Hivyo unaweza kuwa na shida ukakosa kusaidiwa na watu kukupuuza kulingana na lugha au mawasiliano mabovu uliyotumia.

Mwisho, tumia mbinu bora za mawasiliano ili kujenga mahusiano bora na watu waliokuzunguka. Kama mtu anawasiliana na wewe kwa lugha ya Kiswahili usimjibu kwa kingereza.

Friday, September 9, 2016

Mambo 10 Ambayo Mwanaume Hupenda Kusikia Toka Kwa Mpenzi Wake..


10. Kukosolewa – “I think you are wrong”

Wanaume wanaweza kujikweza sana lakini daima hawachukii kurekebishwa. Wanachojali zaidi ni jinsi gani au njia gani imetumika kuwarekebisha. Mwanaume akikosea, anataka mpenzi wake amkosea lakini kwa mapenzi, sio kwa mikwaruzano au dharau au mbele ya kadamnasi. Mrekebishe au mkemee faragha, toa maoni yako na wala usimlazimishe, itamfanya aone unajali na unataka kumjenga.

9. Kujali – “How was your day?”

Wanawake wengi hutaka wao tu ndio waulizwe kuhusu jinsi siku zao zilivyoenda kila siku, wanasahau kabisa hata wanaume nao walikua kwenye mihangaiko. Mzoeshe kumuuliza mpenzi wako siku yake ilikuwaje? utaona hata nuru ya mapenzi yenu itang’aa na mtakua marafiki, japo mwanzoni atakua hakuambii kila kitu lakini baada ya muda atazoea. Kila mtu anataka wa kumsikiliza, mtu atakayezungumza nae chochote kilichotokea ndani ya siku yake, na pengine kukuuliza ushauri.

8. Ucha Mungu – “Can we pray?”

Mwanaume, anayesali au kutosali, lazima huwa ana imani kwamba Mungu yupo. Mwanamke mcha Mungu siku zote huwa ni wazo la kila mwanaume endapo ana mpango wa kuoa. Mwanaume huwa na amani kwa kiasi fulani akiongozwa na mwanamke wake kwa upande huo wa sala.

7.  Msamaha – “I forgive you”

Vikombe kwenye sahani havikosi kugongana, vivyo hivyo na kwa wapenzi, kuumizana hisia hakuepukiki, iwe kwa makusudi au bahati mbaya, mwenzio akikosea sasa isiwe ndo adhabu, akiomba msamaha ukamwambia nimekusamehe na kweli umemsamehe, funika kurasa endeleeni na maisha. Usililete tena mezani jambo ulilosema umesamehe.

6. Sifa – “That was great sex”

Kama amefanya kazi nzuri, mwambie. Wote tunajua sio kila siku watu hufanya kiwango che Maradona au Pele, siku akiwa kwenye kiwango hicho hata yeye anajua, usisite kumpa sifa zake. Wazungu wanasema, ‘Yes, you can kiss and tell some of the times’. Na kama unaona kuna sehemu anahitaji kujisogeza, mwambie pia, tena kimahaba. Hii itawasaida nyote.

5. Upekee  – “I admire you. No other man is like you”

Ni kweli kwamba kuna wanaume ambao ni wazuri na wenye uwezo mkubwa zaidi ya huyo ulienaye, lakini kwake hujisikia vyema zaidi ukimwona yeye ni zaidi ya wote hao. Sio mbele ya macho yake tu, matendo yako na hata nyuma yake msifie kwamba yeye ndio mwanaume pekee duniani unayempenda na hakuna mwingine zaidi yake.

4. Uaminifu – “I trust you”

Mwanaume akijua anaaminika sana kwa mwanamke, na yeye hujiachia. Na kwa hili huwa anaweza kugombana na watu kabisa kwa ajili ya mwanamke wake. Japo wengine hulitumia hili kwa uchafu wao lakini wengi wao ni kitu chema kwao.

3. Mapenzi –  “Make love to me”

Ni mtazamo wa wengi kwamba mwanaume ndio siku zote awe mwanzilishi wa tendo. Lakini mwanaume kwa wakati mwingine hupenda mwanamke wake ampe vishawishi na yeye vya kumleta kwenye mood. Sio kila siku aanze yeye tu, wakati tendo ni la kuwafurahisha wote. Hata kama ni ngumu kusema kwa mwanamke, ishara kibao zipo za kumuonyesha mwenzi wako akaona ‘Leo baby anataka na yeye’.

2. Malengo -“What’s your dream?”

Mwanaume anaweza asionyeshe kama anahitaji msaada, lakini kwa kutumia njia za mapenzi, unakuta ni mwanaume tu anayehitaji uwepo  wa mwanamke anayempenda yeye. Mungu alimtengeneza mwanaume na kumpatia msaidizi kwa kumpatia mwanamke. Kuwa mwanamke mwenye msimamo na mpangilio mahiri usiotikisika, ambaye unauwezo wa kumuuliza anaenda wapi katika maisha yake, na akakukumbusha huko siko ni huku. Ndoto za mwanaume mara nyingi huendana na zile na mwenzi wake, na mwanamke huwa pale kuhakikisha ndoto za pamoja zinatimia.

1. Upendo wa dhati – “I love you”

Wanaume wengi hujiona wagumu kwenye kutamka neno ‘I love you’ kwa wanawake zao na hata akisema itakua ni mara chache chache hata kama kweli kutoka moyoni wanapenda, lakini haina maana hawataki kuambiwa na watu wanaowapenda, hii huwaaminishia nafasi yao kwenye moyo wa mwanamke.

Saturday, September 3, 2016

Serikali Kutoa Ajira Mpya 71,496 Hivi Karibuni


Serikali inatarajia kutoa ajira mpya zipatazo71,496 kwa mwaka huu wa fedha baada ya kukamilika kwa zoezi la kuwaondoa wafanyakazi hewa ambapo hadi sasa watumishi wapatao 839, tayari wapo katika hatua mbalimbali wakiwepoo waliopelekwa katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,(Utumishi na Utawala Bora),Angela Kairuki aliyasema hayo wakati akizungumzia juu ya utekelezaji na mikakati katika Wizara yake katika kipindi cha “Utekelezaji” kinacho rushwa kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania(TBC1).

“Mpaka sasa kuna baadhi ya watumishi hewa waliofanyiwa mahojiano na polisi na kama upelelezi ukikamilika sheria kali zitachukuliwa ikiwepo kufikishwa mahakani kwa mtumishi atakaye bainika kukutwa na makosa “ Alisema Kairuki


Alisema kuwa kuna baadhi ya Maofisa Utumishi pamoja na Wahasibu ambao wameonekana kuwa si waaminifu kwani baadhi yao wameonekana kuelekeza fedha kwa ndugu zao na miradi yao na wengine walishastaafu lakini majina yao yameonekana bado kuendelea kuwepo katika mfumo wa kupokea.

Kairuki aliongeza kuwa katika kipindi cha Machi mosi mpaka kufikia Agosti 20 mwaka huu, Watumishi hewa wapatao 16,127 walibainika ambapo walikuwa wakisababishi hasara ya mabilioni kwa serikali ambapo serikali kama ingewalipa ingesababisha hasara ya zaidi ya bilioni 16.

“Uhakiki huu ni endelevu kwani baadhi ya Maofisa Utumishi pamoja na Wahasibu si waaminifu hivyo tunawataka waajiri wao kuweka mkazo katika swala hili, kwani tunajua wahasibu wengi wamepewa madaraka lakini si waamiifu”Alisema Kiruki.

Kairuki aliwatoa hofu baadhi ya Watanzani ambao walikuwa wakisubiria ajira mpya kutoka Serikali, alisema kuwa kilichokuwa kikisubiriwa ni takwimu halisi ambazo zitasaidia kuonesha ni watumishi wangapi wameweza kuondolewa.

“hii ni neema kwa wanafunzi waliomaliza vyuo kwani kuna nafasi zipatazo 71,496 kwa mwaka huu wa fedha hivyo napenda kuwahauri vijana kuwa na subira kwa kuto kujiingiza katika makundi yasiyo faa” Alisema kairuki.

Pia aliwataka Maofisa Utumishi kuwa hudumia vizuri watumishi kwa kuwapa haki zao ikiwemo kuwa pandisha madaraja kwa wakati stahili na si vema kwa baadhi ya watu kughushi taarifa za Utumishi wa umma na kusisitiza kuwa kufanya hivyo ni kosa kuibwa sana.

Friday, September 2, 2016

TCU Yatangaza Kuanza Udahili Awamu ya PILI Kwa Wanafunzi wanaojiunga Vyuo Vikuu Ambao Wamekosa Nafasi Kwenye Awamu ya Kwanza



Tunapenda kuutangazia Umma kuwa tulifunga mfumo wa pamoja wa udahili tarehe 31/08/2016 saa sita usiku ili kuchakata maombi ya waombaji waliofanikiwa kuomba udahili kwa mwaka wa masomo 2016/2017.
 
Hata hivyo kutokana na wengine kushindwa kufanikiwa kutokana na sababu mbali mbali, Tume inatangaza kuwa itafungua maombi kwa awamu ya pili kuanzia tarehe 12 hadi 23 Septemba 2016 ili kuruhusu makundi yafuatayo kuomba udahili.
  1. Waombaji watakaokuwa wamekosa nafasi kwenye awamu ya kwanza
  2. Waombaji wa kidato cha Sita walioshindwa kuomba katika awamu ya kwanza
  3. Waombaji wenye vigezo vya Stashahada ambao walishindwa kuomba kutokana na matokeo yao kuchelewa kufika NACTE kwa wakati,
  4. Waombaji ambao wamemaliza mitihani ya “Cambridge” mwaka 2016 na matokeo yao yameshatoka,
  5. Waombaji waliofaulu mitihani ya RPL,
  6. Waliokuwa wanafunzi wa vyuo vikuu watakao kuwa na uthibitisho toka vyuo vyao vya awali.
 
Baada ya hapo Tume haitaruhusu tena maombi ili kuruhusu taratibu zingine za kiudahili kuendelea kwa ngazi ya Bodi ya Mikopo na vyuoni.
 
Asanteni
Imetolewa na

Thursday, September 1, 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Azindua Ripoti Ya Hali Ya Hewa Barani Africa


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Afrika wajiulize wanaweza kuchangia kitu gani katika kuboresha maisha ya mamilioni ya wakazi wa bara hilo.

Ametoa kauli hiyo Alhamisi, Agosti 31, 2016 usiku  wakati akizungumza na wawakilishi wa taasisi za kimataifa waliohudhuria uzinduzi wa taarifa ya Taasisi ya Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji barani Afrika (ICF) uliofanyika kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo alisema taasisi hiyo imesaidia kukuza uwekezaji kupitia miradi katika nchi mbalimbali za Afrika kwa kuimarisha mifumo ya ukusanyaji kodi, usajili wa biashara za wajasiriamali na upatikanaji wa leseni za biashara.

“Kutokana na kazi inayofanywa na taasisi hii, hali ya uwekezaji katika nchi nyingi imeimarika na bara la Afrika limekuwa mbia kwa wawekezaji kutokana na ushirikiano baina ya Serikali za nchi husika na sekta binafsi. Uchumi wa nyingi za Afrika umeimarika kuliko hapo awali,” alisema.

Akitoa mfano, Waziri Mkuu alisema zaidi ya wajasiriamali 500 kutoka Tanzania walipatiwa mafunzo kwa ushirikiano baina ya ICF, Serikali na ESAURP ili kuwajengea uwezo waweze kufanya biashara zao kwa tija zaidi. “Mafunzo hayo yaliwalenga wajasiriamali wadogo na wa kati ambao wanajihusisha na uvuvi, biashara za rejereja na jumla kutoka mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam”.

“Kupitia mafunzo hayo, wajasiriamali hao waliweza kusajili biashara, kurasimisha biashara zao, kuongeza mitaji na kujua namna ya kutunza taarifa za biashara zao,” alisema.

Mapema, Mwenyekiti Mwenza wa taasisi hiyo ambaye pia ni Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mhe. Benjamin Mkapa alisema kuna haja ya wananchi kubadili mitazamo yao juu ya sekta binafsi kwani nayo ni muhimu katika ujenzi wa uchumi kwa nchi yoyote ile.

“Watu wengi wanahisi kwamba wawekezaji ni wabaya. Hii si kweli. Tunapaswa kujenga mazingira ya kuwakubali kwa sababu wanakuja na mitaji yao na wao wanawakilisha michango kutoka kwa mamilioni ya wafanyakazi kutoka kwenye nchi zao. Hatupaswi kuwaona kwamba ni maadui,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Mstaafu wa Serikali ya awamu ya nne, Mhe. Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa kukubali kuiruhusu taasisi hiyo ya ICF iweke makao yake makuu hapa nchini wakati ilikuwa imeshakataliwa kufanya hivyo katika nchi nyingi ambako ilipeleka maombi yake.

Aliwataka viongozi mbalimbali watumie uzoefu uliowekezwa na taasisi hiyo kwenye uboreshaji wa mifumo ya mahakama na ukusanyaji kodi, utoaji wa leseni, urasmishaji wa biashara za wajasiriamali wadogo.

“Tunayo maeneo mengi ambayo tumefanya vizuri iwe ni katika TEHAMA, miundombinu, mahakama au mambo ya forodha. Uamuzi ni wenu juu ya jambo lipi muanze nalo katika kuboresha huduma ili kuharakisha maendeleo ya bara hili,” alisema.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

ALHAMISI, SEPTEMBA MOSI, 2016

Mapokezi ya Waziri Mkuu Mjini Dodoma Yaahirishwa Hadi Vikao vya Bunge Viishe



SERIKALI Mkoa wa Dodoma imesema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atahamia rasmi mkoani humo mara baada ya kumalizika kwa vikao vya Bunge vinavyoanza wiki ijayo, Septemba 6.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alisema baada ya kufika Dodoma, ataanza kuratibu utaratibu wa wizara mbalimbali kuhamia katika Makao Makuu hayo ya nchi.

Pamoja na hayo Jeshi la Polisi limejipanga kuongeza vituo vya Polisi ili kuimarisha ulinzi wakati serikali itakapohamia na hakuna mwananchi atakayenyang’anywa ardhi yake kwa sababu yoyote ile.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Rugimbana alisema kama mkoa walishauri ujio huo ufanyike mara baada ya kikao cha Bunge na Waziri Mkuu ameridhia suala hilo.

Alisema Waziri Mkuu atakuwa Mratibu wa wizara zote kuhamia Dodoma na kazi hiyo ataianza rasmi mara baada ya kuwasili mkoani humo.

Alisema maandalizi yanaendelea vizuri na ukarabati wa nyumba ya Waziri Mkuu umefikia asilimia 90.

Alisema Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christine Mndeme aliyekutana na makundi mbalimbali kwa ajili ya mapokezi ya Waziri Mkuu.

“Awali tulisema atakuja Septemba Mosi lakini baada ya kushauriana tumeona aje mara baada ya vikao vya Bunge kwani pilikapilika nyingi zitakuwa zimepungua, kama serikali ikiamua kuja leo tutaipokea kwani maandalizi ya serikali kuja Dodoma yamekamilika kwa asilimia 70,” alisema.