Saturday, September 3, 2016

Serikali Kutoa Ajira Mpya 71,496 Hivi Karibuni


Serikali inatarajia kutoa ajira mpya zipatazo71,496 kwa mwaka huu wa fedha baada ya kukamilika kwa zoezi la kuwaondoa wafanyakazi hewa ambapo hadi sasa watumishi wapatao 839, tayari wapo katika hatua mbalimbali wakiwepoo waliopelekwa katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,(Utumishi na Utawala Bora),Angela Kairuki aliyasema hayo wakati akizungumzia juu ya utekelezaji na mikakati katika Wizara yake katika kipindi cha “Utekelezaji” kinacho rushwa kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania(TBC1).

“Mpaka sasa kuna baadhi ya watumishi hewa waliofanyiwa mahojiano na polisi na kama upelelezi ukikamilika sheria kali zitachukuliwa ikiwepo kufikishwa mahakani kwa mtumishi atakaye bainika kukutwa na makosa “ Alisema Kairuki


Alisema kuwa kuna baadhi ya Maofisa Utumishi pamoja na Wahasibu ambao wameonekana kuwa si waaminifu kwani baadhi yao wameonekana kuelekeza fedha kwa ndugu zao na miradi yao na wengine walishastaafu lakini majina yao yameonekana bado kuendelea kuwepo katika mfumo wa kupokea.

Kairuki aliongeza kuwa katika kipindi cha Machi mosi mpaka kufikia Agosti 20 mwaka huu, Watumishi hewa wapatao 16,127 walibainika ambapo walikuwa wakisababishi hasara ya mabilioni kwa serikali ambapo serikali kama ingewalipa ingesababisha hasara ya zaidi ya bilioni 16.

“Uhakiki huu ni endelevu kwani baadhi ya Maofisa Utumishi pamoja na Wahasibu si waaminifu hivyo tunawataka waajiri wao kuweka mkazo katika swala hili, kwani tunajua wahasibu wengi wamepewa madaraka lakini si waamiifu”Alisema Kiruki.

Kairuki aliwatoa hofu baadhi ya Watanzani ambao walikuwa wakisubiria ajira mpya kutoka Serikali, alisema kuwa kilichokuwa kikisubiriwa ni takwimu halisi ambazo zitasaidia kuonesha ni watumishi wangapi wameweza kuondolewa.

“hii ni neema kwa wanafunzi waliomaliza vyuo kwani kuna nafasi zipatazo 71,496 kwa mwaka huu wa fedha hivyo napenda kuwahauri vijana kuwa na subira kwa kuto kujiingiza katika makundi yasiyo faa” Alisema kairuki.

Pia aliwataka Maofisa Utumishi kuwa hudumia vizuri watumishi kwa kuwapa haki zao ikiwemo kuwa pandisha madaraja kwa wakati stahili na si vema kwa baadhi ya watu kughushi taarifa za Utumishi wa umma na kusisitiza kuwa kufanya hivyo ni kosa kuibwa sana.

Friday, September 2, 2016

TCU Yatangaza Kuanza Udahili Awamu ya PILI Kwa Wanafunzi wanaojiunga Vyuo Vikuu Ambao Wamekosa Nafasi Kwenye Awamu ya Kwanza



Tunapenda kuutangazia Umma kuwa tulifunga mfumo wa pamoja wa udahili tarehe 31/08/2016 saa sita usiku ili kuchakata maombi ya waombaji waliofanikiwa kuomba udahili kwa mwaka wa masomo 2016/2017.
 
Hata hivyo kutokana na wengine kushindwa kufanikiwa kutokana na sababu mbali mbali, Tume inatangaza kuwa itafungua maombi kwa awamu ya pili kuanzia tarehe 12 hadi 23 Septemba 2016 ili kuruhusu makundi yafuatayo kuomba udahili.
  1. Waombaji watakaokuwa wamekosa nafasi kwenye awamu ya kwanza
  2. Waombaji wa kidato cha Sita walioshindwa kuomba katika awamu ya kwanza
  3. Waombaji wenye vigezo vya Stashahada ambao walishindwa kuomba kutokana na matokeo yao kuchelewa kufika NACTE kwa wakati,
  4. Waombaji ambao wamemaliza mitihani ya “Cambridge” mwaka 2016 na matokeo yao yameshatoka,
  5. Waombaji waliofaulu mitihani ya RPL,
  6. Waliokuwa wanafunzi wa vyuo vikuu watakao kuwa na uthibitisho toka vyuo vyao vya awali.
 
Baada ya hapo Tume haitaruhusu tena maombi ili kuruhusu taratibu zingine za kiudahili kuendelea kwa ngazi ya Bodi ya Mikopo na vyuoni.
 
Asanteni
Imetolewa na

Thursday, September 1, 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Azindua Ripoti Ya Hali Ya Hewa Barani Africa


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Afrika wajiulize wanaweza kuchangia kitu gani katika kuboresha maisha ya mamilioni ya wakazi wa bara hilo.

Ametoa kauli hiyo Alhamisi, Agosti 31, 2016 usiku  wakati akizungumza na wawakilishi wa taasisi za kimataifa waliohudhuria uzinduzi wa taarifa ya Taasisi ya Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji barani Afrika (ICF) uliofanyika kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo alisema taasisi hiyo imesaidia kukuza uwekezaji kupitia miradi katika nchi mbalimbali za Afrika kwa kuimarisha mifumo ya ukusanyaji kodi, usajili wa biashara za wajasiriamali na upatikanaji wa leseni za biashara.

“Kutokana na kazi inayofanywa na taasisi hii, hali ya uwekezaji katika nchi nyingi imeimarika na bara la Afrika limekuwa mbia kwa wawekezaji kutokana na ushirikiano baina ya Serikali za nchi husika na sekta binafsi. Uchumi wa nyingi za Afrika umeimarika kuliko hapo awali,” alisema.

Akitoa mfano, Waziri Mkuu alisema zaidi ya wajasiriamali 500 kutoka Tanzania walipatiwa mafunzo kwa ushirikiano baina ya ICF, Serikali na ESAURP ili kuwajengea uwezo waweze kufanya biashara zao kwa tija zaidi. “Mafunzo hayo yaliwalenga wajasiriamali wadogo na wa kati ambao wanajihusisha na uvuvi, biashara za rejereja na jumla kutoka mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam”.

“Kupitia mafunzo hayo, wajasiriamali hao waliweza kusajili biashara, kurasimisha biashara zao, kuongeza mitaji na kujua namna ya kutunza taarifa za biashara zao,” alisema.

Mapema, Mwenyekiti Mwenza wa taasisi hiyo ambaye pia ni Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mhe. Benjamin Mkapa alisema kuna haja ya wananchi kubadili mitazamo yao juu ya sekta binafsi kwani nayo ni muhimu katika ujenzi wa uchumi kwa nchi yoyote ile.

“Watu wengi wanahisi kwamba wawekezaji ni wabaya. Hii si kweli. Tunapaswa kujenga mazingira ya kuwakubali kwa sababu wanakuja na mitaji yao na wao wanawakilisha michango kutoka kwa mamilioni ya wafanyakazi kutoka kwenye nchi zao. Hatupaswi kuwaona kwamba ni maadui,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Mstaafu wa Serikali ya awamu ya nne, Mhe. Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa kukubali kuiruhusu taasisi hiyo ya ICF iweke makao yake makuu hapa nchini wakati ilikuwa imeshakataliwa kufanya hivyo katika nchi nyingi ambako ilipeleka maombi yake.

Aliwataka viongozi mbalimbali watumie uzoefu uliowekezwa na taasisi hiyo kwenye uboreshaji wa mifumo ya mahakama na ukusanyaji kodi, utoaji wa leseni, urasmishaji wa biashara za wajasiriamali wadogo.

“Tunayo maeneo mengi ambayo tumefanya vizuri iwe ni katika TEHAMA, miundombinu, mahakama au mambo ya forodha. Uamuzi ni wenu juu ya jambo lipi muanze nalo katika kuboresha huduma ili kuharakisha maendeleo ya bara hili,” alisema.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

ALHAMISI, SEPTEMBA MOSI, 2016

Mapokezi ya Waziri Mkuu Mjini Dodoma Yaahirishwa Hadi Vikao vya Bunge Viishe



SERIKALI Mkoa wa Dodoma imesema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atahamia rasmi mkoani humo mara baada ya kumalizika kwa vikao vya Bunge vinavyoanza wiki ijayo, Septemba 6.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alisema baada ya kufika Dodoma, ataanza kuratibu utaratibu wa wizara mbalimbali kuhamia katika Makao Makuu hayo ya nchi.

Pamoja na hayo Jeshi la Polisi limejipanga kuongeza vituo vya Polisi ili kuimarisha ulinzi wakati serikali itakapohamia na hakuna mwananchi atakayenyang’anywa ardhi yake kwa sababu yoyote ile.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Rugimbana alisema kama mkoa walishauri ujio huo ufanyike mara baada ya kikao cha Bunge na Waziri Mkuu ameridhia suala hilo.

Alisema Waziri Mkuu atakuwa Mratibu wa wizara zote kuhamia Dodoma na kazi hiyo ataianza rasmi mara baada ya kuwasili mkoani humo.

Alisema maandalizi yanaendelea vizuri na ukarabati wa nyumba ya Waziri Mkuu umefikia asilimia 90.

Alisema Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christine Mndeme aliyekutana na makundi mbalimbali kwa ajili ya mapokezi ya Waziri Mkuu.

“Awali tulisema atakuja Septemba Mosi lakini baada ya kushauriana tumeona aje mara baada ya vikao vya Bunge kwani pilikapilika nyingi zitakuwa zimepungua, kama serikali ikiamua kuja leo tutaipokea kwani maandalizi ya serikali kuja Dodoma yamekamilika kwa asilimia 70,” alisema.

UVCCM yaivaa rasmi Chadema kwa kushindwa kufanya Maandamano ya UKUTA


Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), umewavaa viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kile walichodai kuendesha siasa za maigizo baada ya kushindwa kuzindua Operesheni UKUTA, Septemba 1.

Kupitia taaria yake kwa vyombo vya habari, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, amesema kuwa Chadema walijua kuwa hawana ubavu wa kufanya maandamano na mikutano nchi nzima Septemba 1 na kwamba walichofanya ni kuwatia hofu wananchi.

“UVCCM tulijua, tulielewa na kutambua bayana kwamba Chadema walikuwa wanafanya maigizo katika siasa, hawana ubavu wala jeuri ya kuandamana kwa madai ya kipuuzi na ambayo sio ya msingi kwa mustakabali wa nchi yetu,” alisema Shaka.

Aidha, Shaka alikanusha sababu zilizotolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuahirisha maandamano hayo kuwa wameombwa na viongozi wa dini ili waweze kukaa na pande zote kujaribu kutafuta suluhu kwa amani.

“UVCCM inatamka bayana kuwa hakuna majadiliano, mazungumzo wala mijadala itakayojadiliwa kati ya Serikali ya CCM na Chadema. Tunaomba Serikali ya Rais John Magufuli iendelee na mikakati yake ya kisera,” Shaka ameongeza.

Kaimu Katibu Mkuu huyo wa UVCCM alisisitiza kuwa Chadema hawana ubavu wa kufanya maandamano na mikuano nchi nzima Oktoba 1 kama walivyosema, baada ya kushindwa kufanya hivyo Septemba 1.

Shaka amesema wanachokifanya hivi sasa Chadema kinatokana na kushindwa kubuni mikakati ya kufanya siasa ili chama chao kiimarike na kukubarika.

Juzi, Chadema walitangaza kuahirisha uzinduzi wa oparesheni UKUTA nchi nzima, iliyokuwa imepangwa kufanyika jana (Septemba 1) kwa maandamano na mikutano nchi nzima.

UVCCM pia walitangaza kuahirisha maandamano yao ya nchi nzima waliyokuwa wamepanga kuyafanya Agosti 31 kwa lengo la kumpongeza Rais Magufuli kwa kazi aliyoifanya ndani ya kipindi kifupi.

Maandamano ya pande zote mbili yalipigwa marufuku na Jeshi la Polisi nchini.