KATIBU
wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amesema
kasi ya utendaji kazi ya Rais John Magufuli inaweza kuua uwepo wa vyama
vya upinzani nchini.
Hata
hivyo alisema kuwa hangependa upinzani ufe kwa vile hiyo pia itakuwa
imeua demokrasia nchini na kudai kuwa lengo la kuanzisha vyama vya siasa
haikuwa kuviua bali ni kuviona vikiendelea kuwepo.
Kauli
hiyo ilitolewa juzi na Katibu huyo wakati alipokuwa akikagua maandalizi
ya Maadhimisho ya Sherehe ya miaka 39 ya CCM ambayo kilele chake
kimepangwa kufanyika mkoani hapa Februari 6, mwaka huu badala ya
Februari 5 iliyozoeleka.
Alisema
kuwa chama kimelazimika kubadili tarehe ya kilele ili kuwawezesha
wananchi kushiriki ipasavyo maadhimisho hayo kwa kufanya kazi badala ya
kuwa na sherehe mbalimbali.
“Maadhimisho
ya safari hii ni tofauti na ya miaka mingine. Safari hii wananchi
watatakiwa kushiriki zaidi kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo.
Kauli mbiu yetu ni ‘Sasa kazi’ hivyo watu wafanye kazi ili wajiletee
maendeleo yao wenyewe,” alisema.
No comments:
Post a Comment