Jeshi
la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata watu wengine
wawili, akiwamo mpenzi wa mfanyakazi wa ndani wa Aneth Msuya, aliyeuawa
kwa kuchinjwa nyumbani kwake.
Aneth,
ambaye ni dada wa Bilionea Erasto Msuya, aliuawa kwa kuchinjwa na watu
wasiojulikana Mei 26 nyumbani kwake Kibada, Kigamboni jijini Dar es
Salaam.
Wauaji
hao hawakuchukua chochote kwenye nyumba hiyo. Bilionea Msuya aliuawa
Agosti mwaka jana kwa kupigwa risasi na tayari watu 12 wamekatwa,
wakituhumiwa kuhusika na mauaji hayo.
Kamanda
wa Kanda hiyo, Simon Sirro alisema hadi sasa wamekamata watuhumiwa
wanne wakihusishwa na mauaji ya dada wa bilionea huyo.
Kati
ya watuhumiwa waliokamatwa, yumo mume wa Aneth, msaidizi wa ndani wa
Aneth na mtuhumiwa mwingine ambaye Kamanda Sirro hakumtaja jina.
“Mwanzo
tulimkamata mume wa marehemu na msaidizi wa ndani wa marehemu, lakini
sasa wameongezeka wengine wawili, akiwamo hawara wa msaidizi wa ndani.
Tunaendelea kuwahoji na upelelezi ukikamilika tutawafikisha mahakamani,” alisema Sirro.
Kwa
mujibu wa mama mdogo wa marehemu, Lilian Benjamin, msaidizi wa ndani wa
dada wa bilionea huyo aliondoka saa sita mchana na kuacha funguo nyumba
ya jirani.
Lilian alisema msaidizi huyo alimpigia simu ghafla bosi wake mchana na kumwambia anaondoka na hataendelea na kazi.
Mauaji
ya Aneth ni mwendelezo wa mauaji yanayoikumba familia hiyo ya Msuya
baada ya kaka yake, Erasto ambaye alikuwa ni mfanyabiashara tajiri wa
madini, kuuawa Agosti 7, 2013 kwa kupigwa risasi zaidi ya 12 kwa kutumia
bunduki ya SMG katika eneo la Mijohoroni wilayani Hai, Mkoa wa
Kilimanjaro.
Februari
10, mawakili wanaosimamia kesi ya Erasto, Hudson Ndusyepo, Majura
Magafu, Emanuel Safari na John Lundu, waliiambia mahakama kuwa Serikali
inakusudia kuita mashahidi 50 kuthibitisha shtaka hilo na kuwasilisha
vielelezo 40, ikiwamo bunduki hiyo.
Mawakili
hao walidai mipango ya kumuua bilionea Msuya ilianza Julai 26,2013
jijini Arusha, ikiwahusisha washtakiwa na waliotekeleza mauaji hayo
wangelipwa Sh5 milioni kila mmoja.
Wakitoa
maelezo ya tukio hilo, mawakili hao waliiambia mahakama kuwa washiriki
ambao wasingeenda moja kwa moja kwenye mauaji, wao wangelipwa Sh3
milioni kila mmoja.
Mshtakiwa wa kwanza, Shariff Mohamed anadaiwa kuwa ndiye alikuwa mpangaji mkuu na alitoa fedha za maandalizi yote ya mauaji.
Washtakiwa
wengine ni Shaibu Jumanne, ambaye anafahamika kwa jina la utani la
Mredii, Mussa Mangu, Jalila Zuberi (Said), Karim Kihundwa, Sadick Jabir
(Msudani) na Ally Mussa (Mjeshi).
No comments:
Post a Comment