Kauli
ya mwanahabari nguli nchini, Jenerali Ulimwengu kutaka Rais Mstaafu
Jakaya Kikwete ashtakiwe mahakamani kwa kuitia hasara Serikali imeibua
mjadala mzito, huku wasomi wakisema ipo haja ya kubadili Katiba ili mkuu
wa nchi aweze kushtakiwa baada ya kuondoka madarakani.
Wasomi
hao walisema ile kauli ya “hakuna aliye juu ya sheria” inapaswa
kufuatwa na watu wote, wakitolea mfano Rais wa Brazil, Dilma Roussef
aliyeng’olewa na Bunge baada ya kutuhumiwa kukiuka sheria za usimamizi
wa akaunti ya bajeti ya nchi hiyo.
Kwa sasa nafasi yake inashikiliwa na aliyekuwa makamu wake, Michel Temer.
Kwa sasa nafasi yake inashikiliwa na aliyekuwa makamu wake, Michel Temer.
Hata hivyo, baadhi ya wasomi wamesema jukumu hilo la kumshtaki rais mstaafu inafaa liachwe mikononi mwa Bunge.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 imempa kinga rais mstaafu ya kushtakiwa kwa jambo lolote alilofanya alipokuwa madarakani na imetoa mlolongo mrefu rais aliyeko madarakani kuondolewa.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 imempa kinga rais mstaafu ya kushtakiwa kwa jambo lolote alilofanya alipokuwa madarakani na imetoa mlolongo mrefu rais aliyeko madarakani kuondolewa.
Juzi
wakati akizungumza katika Tamasha la Nane la Kigoda cha Mwalimu
Nyerere, Jenerali ambaye pia ni mwanasheria wa kujitegemea alisema
Kikwete anapaswa kushtakiwa kwa kuisababishia hasara Serikali kutokana
na kuruhusu mabilioni ya shilingi kutumika katika mchakato wa Katiba
ambayo haikupatikana.
Mbali
na fedha zilizotumiwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakati wa
kukusanya maoni, kununulia magari, kulipia pango la ofisi, nyingine
zilitumika kurekebisha ukumbi wa Bunge uweze kubeba wajumbe wa Bunge
Maalum la Katiba, na kulipa posho ya Sh300,000 kwa siku kwa wajumbe 620
kwa muda wa siku 130.
“Itabidi
(Kigoda cha Mwalimu) mumuite (Kikwete) mwaka ujao, aje aeleze fedha za
wananchi zilizotumika katika mchakato ule zilikuwa na sababu gani,” alisema huku akishangiliwa na umati wa watu.
Jenerali
aliyewahi kuwa mkuu wa wilaya za Hai na Ilala na mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya Taifa ya CCM, alisema kama mawaziri wa zamani wamepandishwa
kizimbani kwa kusababisha hasara, hata Kikwete anapaswa kupelekwa
mahakamani kwa kusababisha hasara kwa Serikali na kuzima matumaini ya
wananchi, jambo linaloweza kusababisha machafuko nchini.
Ibara
ya 46 sehemu ya (1) ya Katiba inasema wakati wote Rais atakapokuwa bado
ameshika madaraka yake kwa mujibu wa Katiba hii, itakuwa ni marufuku
kumshitaki au kuendesha mashataka ya aina yoyote juu yake mahakamani kwa
ajili ya kosa lolote la jinai.
Sehemu
ya (3) inasema isipokuwa kama ataacha kushika madaraka ya Rais kutokana
na masharti ya ibara ya 46A (10), itakuwa ni marufuku kumshtaki au
kufungua mahakamani shauri lolote la jinai au la kumdai mtu aliyekuwa
anashika madaraka ya Rais baada ya kuacha madaraka hayo kutokana na
jambo lolote alilofanya yeye kama Rais wakati alipokuwa bado anashika
madaraka ya Rais kwa mujibu wa Katiba hii.
Ibara
ya 46A sehemu ya (1) inasema bila ya kujali masharti ya ibara ya 46 ya
Katiba hii, Bunge linaweza kupitisha azimio la kumuondoa Rais madarakani
endapo itatolewa hoja ya kumshtaki Rais na ikapitishwa kwa mujibu wa
masharti ya ibara hii.
Sehemu
ya (2) imeweka masharti kwamba bila ya kuathiri masharti mengineyo ya
ibara hii, hoja yoyote ya kumshtaki Rais haitatolewa isipokuwa tu kama
inadaiwa kwamba Rais; (a) ametenda vitendo ambavyo kwa jumla vinaivunja
Katiba au Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma; (b) ametenda vitendo
ambavyo vinakiuka maadili yanayohusu uandikishwaji wa vyama vya siasa
yaliyotajwa katika ibara ya 20 (2) ya Katiba.
Mbali
ya Katiba ya sasa kumwekea kinga Rais mstaafu, Rasimu ya Mabadiliko ya
Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba na Katiba
Inayopendekezwa zilinakiri kipengele hicho kinachompa Rais mstaafu kinga
ya kutoshtakiwa bila kubadili chochote.
Maoni ya wasomi
Mhadhiri wa Shule ya Siasa ya Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk James Jesse alisema ili kuondoa kile alichokiita ‘kusumbuliwa’, jukumu la kumshtaki Rais mstaafu au aliyepo madarakani linapaswa kuachwa mikononi mwa Bunge.
Maoni ya wasomi
Mhadhiri wa Shule ya Siasa ya Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk James Jesse alisema ili kuondoa kile alichokiita ‘kusumbuliwa’, jukumu la kumshtaki Rais mstaafu au aliyepo madarakani linapaswa kuachwa mikononi mwa Bunge.
“Katiba
imeeleza wazi kwamba ataondolewa madarakani kwa azimio la Bunge.
Binafsi nadhani utaratibu huo ndiyo mzuri hata kama atakuwa amemaliza
muda wake, hoja ya kumshtaki ianzie bungeni,” alisema .
Naye Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Innocent Shoo alisema,
“Tukizingatia demokrasia za kisasa, rais akitoka madarakani hapaswi
kuwa na kinga ya kushtakiwa. Hii inatakiwa iwezekane hata akiwa
madarakani ili kuzingatia utawala wa sheria.”
Katika
ufafanuzi wake, Shoo alisema kuwa kutokuwajibika na utamaduni wa
kutokujali ni utambulisho wa viongozi wengi barani Afrika huku akinukuu
kauli ya Rais wa Marekani, Barack Obama, kwamba “Afrika inatakiwa kuwa
na taasisi imara siyo mwanaume mwenye nguvu.”
Shoo
alisema nchi nyingi barani Afrika hazina chaguzi huru, haziheshimu haki
za binadamu na uhuru wa watu na taasisi mbalimbali, mambo aliyodai kuwa
yanafaa kumfanya Rais kushtakiwa.
“Umeona
kilichotokea Brazil? Ule ni mfano hai kuwa rais anaposhindwa kufuata
sheria na taratibu ashtakiwe tena ashtakiwe hata akiwa madarakani,” alisisitiza.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua), Profesa Damian Gabagambi alisema, “Anapaswa kushtakiwa anapomaliza utawala wake na hasa kama wakati akiwa rais alikuwa akifanya mambo ya kulihujumu taifa.”
Profesa
Gabagambi ambaye alikuwa mmoja wa wataalamu walioandaa Mpango wa
Matokeo Makubwa Sasa (BRN), alisema kushtakiwa siyo kufungwa kwa kuwa
mtuhumiwa atakwenda mahakamani na kujitetea.
“Hii
itasaidia viongozi wakati wa utawala wao kuheshimu utawala bora na
kufuata sheria na Katiba ili kukwepa kushtakiwa, mara wamalizapo kipindi
chao cha kuongoza,” alisema.
Naibu
Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch alisema
Katiba inampa Rais kinga ya maisha, jambo ambalo si sahihi huku akieleza
kuwa wazo la Kikwete la kuanzisha mchakato wa kuandika Katiba Mpya
lilikuwa zuri ila liliharibiwa na wanasiasa.
“Kinga
aliyonayo rais ndiyo inayompa kiburi na ndiyo sababu akiwa madarakani
akishauriwa hataki, ila akimaliza muda wake anajuta kwa uamuzi
aliouchukua,” alisema Olouch huku akisisitiza kuwa hayo ni maoni yake binafsi si ya CWT.
Akitolea
mfano wa kilichomkumba Rais wa Brazil, Oluoch ambaye alikuwa mjumbe wa
Bunge Maalum la Katiba, alisema hata kama nchi nyingine nazo zina kinga
kwa marais wao, si lazima Tanzania kubaki na kinga hiyo kwa kuwa kila
nchi ina utamaduni na ustaarabu wake.
“Rais
wa Tanzania yupo juu ya sheria. Mfano Benjamin (MkapaRais wa Awamu ya
Tatu) amesema anajutia uamuzi wake wa ubinafsishaji na kutowekeza katika
elimu. Hayo ni baadhi tu ya makosa wanayoyafanya viongozi wetu,” alisema Oluoch.
Makamu
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala alisema
kuondoa kinga ya Rais baada ya utawala wake ni hatari kwa usalama na
demokrasia ya nchi.
Alisema
kwa kuwa kila kiongozi hufanya maamuzi ya kisiasa ambayo wakati
mwingine hayatimii, kuondolewa kwa kinga hiyo kunaweza kukaleta matatizo
ya kisiasa kwa siku za mbele.
“Kuna mtu atakuja kung’ang’ania ikulu endapo atatambua kuwa yupo kwenye hatari ya kufikishwa mahakamani,”
alisema Profesa Mukandala na akashauri zianzishwe taasisi makini na
imara zitakazokuwa zinamshauri Rais juu ya maamuzi mbalimbali
anayoyafanya akiwa madarakani.
Alisema
hakuna haja ya kuwafikisha mahakamani viongozi wa ngazi hiyo, kama
makosa yao yalitokana na mtazamo wa kisiasa na kukumbusha kuwa hata Rais
wa awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere alishindwa kutekeleza
mkakati wa kuanzisha Vijiji vya Ujamaa kama ulivyoratibiwa sawa na
ilivyotokea kwenye Katiba Mpya kipindi cha Rais Kikwete.
Chama
cha Wananchi (CUF) Zanzibar, kimeunga mkono kauli ya Jenerali kuhusu
Kikwete kushtakiwa kuhusiana na mchakato wa Katiba ambayo
haikupatikana.
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salim Bimani alisema CUF inaunga mkono kwa asilimia 100 kauli hiyo, kwa sababu sehemu kubwa ya matatizo yaliyojitokeza na yanayojitokeza Zanzibar yamesababishwa na kutopatikana kwa Katiba Mpya.
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salim Bimani alisema CUF inaunga mkono kwa asilimia 100 kauli hiyo, kwa sababu sehemu kubwa ya matatizo yaliyojitokeza na yanayojitokeza Zanzibar yamesababishwa na kutopatikana kwa Katiba Mpya.
“CUF
tungekuwa na uwezo hata leo tungetaka ashtakiwe haraka iwezekanavyo.
Kwa sababu Kikwete ni mmoja wa watu aliyevuruga uchaguzi Oktoba 25,
mwaka jana,” alisema Bimani.
Lakini
Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Vua Ali Vuai alisema maoni ya
Jenerali si sahihi na si ya kiungwana kwa kuwa yana lengo la kuleta
uchochezi kwa wananchi dhidi ya Kikwete.
“Huu
ni upotoshaji kwa wananchi, kwa sababu Kikwete amefanya mambo makubwa
nchini. Sioni sababu ya kusema fedha nyingi zimetumika wakati mchakato
huu bado unaendelea, ukisubiri kupiga kura za maoni.
No comments:
Post a Comment