MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imetengua matokeo ya kiti
cha diwani wa Kata ya Saranga, Efraim Kinyafu (CHADEMA), baada ya
kubaini kwamba uchaguzi ulikiuka taratibu katika kuhesabu kura.
Kesi
hiyo ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa nafasi hiyo kupitia Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Yusuf Mdoe dhidi ya diwani huyo Kinyafu na msimamizi
wa uchaguzi wa kata hiyo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Hukumu
hiyo imetolewa leo mahakamani hapo na Hakimu Mkazi Mkuu, Warialwande
Lema ambaye kwa sasa amehamishiwa kituo kingine cha kazi na ilisomwa kwa
niaba yake na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.
“Mahakama
baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na pande zote mbili, imebaini
kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu katika kuhesabu kura inatengua
matokeo ya uchaguzi wa kata ya Saranga” alisema Hakimu Mashauri.
Mdoe
alifungua kesi hiyo akidai kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu za
kuhesabu kura akilalamikia kituo kimoja na kuiomba mahakama kuamua
vyovyote itakavyoona inafaa na itamke uchaguzi haukuwa wa huru na wa
haki.
Akizungumza
baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili Fredrick Kihwelu, alidai
mteja wake hajaridhika na hukumu hiyo hivyo watakata rufani kuipinga.
Alidai wataomba mahakamani wapatiwe mwenendo wa kesi ili waweze kuwasilisha sababu za kukata rufani.
Wakili
huyo alidai mdai huyo alikuwa halalamikii kushindwa kwa kuwa wakati wa
usikilizwaji wa shauri hilo, alikiri kushindwa kwa tofauti ya kura zaidi
ya 500.
Alidai
katika kituo ambacho alikuwa akilalamikia mdai huyo kulikuwa na
wapigakura 68, hivyo hata kama kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu za
kuhesabu kura kusingeweza kubadili matokeo yote.
Wakili
huyo alishauri kwamba aliyepaswa kusahihishwa kwa kukiuka taratibu ni
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kesho na keshokutwa iwe makini kwa
kutorudia makosa na sio mdaiwa wa kwanza (Kinyafu).
No comments:
Post a Comment