Mwanahabari
nguli nchini Jenerali Ulimwengu amesema Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete
anapaswa kushtakiwa mahakamani kwa kuisababishia hasara Serikali
kutokana na mabilioni ya shilingi yaliyotumika katika mchakato wa Katiba
ambayo haikupatikana.
Akizungumza katika tamasha la nane la Kigoda cha Mwalimu Nyerere katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) jana, Jenerali Ulimwengu alisema fedha nyingi zimepotea wakati wa kuunda Katiba Mpya ambayo haikupatikana.
Mbali
ya fedha zilizotumika na Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakati wa
kukusanya maoni na nyingine zilizotumika kurekebisha ukumbi wa Bunge
uweze kubeba wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, jumla ya Sh24.53
bilioni zilitumika kulipa posho za wajumbe.
Tamasha
hilo lililojikita kujadili falsafa za Mwalimu Nyerere katika muktadha
wa “Visheni ya Maendeleo ya Watu,” liliwakutanisha wasomi mbalimbali
kutoka ndani na nje ya nchi, wanafunzi na wanasiasa wakiwamo Katibu Mkuu
wa CCM, Abdulrahman Kinana na Waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph
Warioba.
Jenerali
aliyekuwa anajadili hotuba ya mgeni rasmi, Benjamin Mkapa, alisema
fedha nyingi ziligharamia mchakato wa Katiba uliokuwa unaendeshwa na
Tume ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba, lakini ulikwama, ndiyo
maana hadi leo hakuna Katiba mpya.
“Itabidi
(Kigoda cha Mwalimu) mumuite mwaka ujao, aje aeleze fedha za wananchi
zilizotumika katika mchakato ule zilikuwa na sababu gani,” alisema Jenerali aliyekuwa akishangiliwa na wahudhuriaji.
“Iwapo
mawaziri wa zamani wamechukuliwa hatua na kupelekwa mahakamani kwa
kusababisha hasara, Mheshimiwa Kikwete anastahili kupelekwa mahakamani
kwa kusababisha hasara kwa Serikali na kuzima matumaini ya wananchi na
kuachwa wanarandaranda wasijue wafanye nini na baadaye inaweza kutuletea
machafuko, kama hatukuweza kutengeneza Katiba ambayo itatuwekea
mustakbali wa Watanzania,” alisema.
Jenerali alisema suala la Katiba limekwama na limekwamishwa kwa makusudi kabisa.
Kuhusu
Mwalimu Nyerere, Jenerali alisema asingekuwa anazungumzwa kwa sifa
nyingi kama sasa, iwapo asingechukua uamuzi wa mwaka 1992 wa kuruhusu
mfumo wa vyama vingi, licha ya kwamba waliokuwa wameukubali ni asilimia
20 ya Watanzania.
Kuhusu
Rais John Magufuli, Jenerali alisema pamoja na sifa anazopewa sasa za
utendaji wake, akitazamwa kwa uwanda mpana, nchi imerudi nyuma kwa miaka
50 kwa masuala ya demokrasia.
Akifafanua namna nchi ilivyorudi nyuma, alisema, “Kwa kufinya uhuru wa kujieleza na hususan kwa kufinya uhuru wa wawakilishi wa wananchi ndani ya Bunge.”
Baadaye,
Rais mstaafu, Benjamin Mkapa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika tamasha
hilo alifafanua kauli ya Jenerali kwa kusema yeye (Mkapa) hakuwa mshauri
wa Rais, bali Jaji Warioba alimfuata atoe ushauri na hakuwa kwenye
ngazi yoyote ya uamuzi.
“Kwenye chama changu sikuwemo na kwenye Serikali sikuwemo. Siwezi kulizunguzumzia hilo na waandishi wanapenda nitoe maoni,” alisema Mkapa.
Alisema ipo haja ya kujiuliza kwa nini Katiba hiyo ilikwama na hadi sasa hajasikia uchambuzi wa kina kuhusu jambo hilo.
“Kuna
haja ya kuwa na mjadala mkubwa lakini siyo kulaumiana tu. Siyo kudai
tu. Kuwezesha uhuru wa kuzungumza ni jambo moja na kutumia uhuru huo ni
kujadili, kuchambua na kupima na kufanya uamuzi sahihi kitu kingine
kabisa,”alisema Mkapa.
Alisisitiza kuwa badala ya kumlaumu mtu mmoja mmoja, mjadala mpana wa kitaifa unahitajika ili kujua kilichosababisha Taifa kukosa Katiba Mpya.
“Hakuna
anayeandika ni wapi tulipokwama, tunalaumu na kumjadili mtu, wengine
wanasema Katiba imekwamishwa na watu wachache kwa sababu za
kimaslahi…tunapaswa kuwa na mjadala wa kina kujua ni wapi tulipokwama,” alisema Mkapa.
Aidha,
Jenerali aliwananga viongozi wastaafu akisema amebaini sasa kuwa kwa
bahati mbaya wanapata busara baada ya kuacha nafasi za uongozi.
Alisema
ili kuwa na busara wakati mtu akiwa madarakani, anatakiwa awasikilize
wale anaowaongoza na njia moja ya kufanya hivyo ni kuwapa Katiba ambayo
ndiyo mwongozo utakaosimamia mustakabali wao.
Awali,
akiwasilisha mada katika tamasha hilo, Mkapa alisema si kana kwamba
Mwalimu Nyerere hakupenda kampuni binafsi zije kuwekeza nchini bali
alipenda biashara na uwekezaji vifanyike kwa haki, usawa na kuchangia
maendeleo ya nchi.
Kuhusu
sukari, Mkapa ambaye alijitetea kwa kuanzisha sera ya ubinafsishaji,
alisema wakati anaingia madarakani, viwanda vya sukari vikiwamo
Kilombero na Mtibwa vilikuwa havizalishi kabisa au kuzalisha kidogo,
hivyo kulikuwa na tatizo la sukari.
Alisema
baada ya ubinafsishaji, sukari ilianza kuzalishwa kwa wingi lakini
akahoji ni nini hakikufanyika hadi nchi ikafikia mahali ilipo sasa.
Ugawaji mikoa
Akichangia
mjadala huo, mhadhiri mwandamizi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili
(Tataki) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Martha Qorro alisema
Serikali imeendelea kuongeza idadi ya mikoa, jambo ambalo linazidi
kuwagawa wananchi.
Pamoja
na kuathiri umoja wa kitaifa, mhadhiri huyo alikuwa na maoni kuwa,
fedha nyingi kwa sasa zinatumika kuendesha mikoa inayoongezwa badala ya
kuleta maendeleo kwa wananchi.
Hata
hivyo, Mkapa alisema wakati wa uongozi wake aliongeza mkoa mmoja tu wa
Manyara, ambao aliumega kutoka Arusha baada ya kuona uhitaji na kufanya
vikao.
Rais
huyo mstaafu alisema suala la kuzingatia wakati wa ugawaji wa mikoa ni
kutowagawa wananchi kwa misingi ya ukabila na udini.
Mstaafu
huyo aliyeiongoza nchi kipindi cha mwaka 1995-2005, alisema suala la
kuangalia ni mahitaji ya watu ndiyo maana alikaa na viongozi wa maeneo
yote hayo na hatimaye kufanikiwa kuigawa Arusha.
Alisema
Watanzania wengi wamekuwa na desturi ya kutumia muda mwingi katika
kuilaumu Serikali badala ya kufanya kazi kwa maendeleo ya nchi.
“Watanzania
tunatakiwa tufanye kazi kwa bidii ili tuifikishe nchi yetu kwenye
maendeleo na si kutumia muda mwingi katika kuilaumu Serikali,” alisema Mkapa.
No comments:
Post a Comment