TAASISI
ya Twaweza imetoa matokeo ya utafiti wake, ambapo imebainika kuwa
asilimia 79 ya Watanzania wamepinga uamuzi wa Serikali wa kusitisha
matangazo ya moja kwa moja (Live ) ya Bunge.
Katika maoni yao, wananchi hao wamedai kuwa ni haki yao ya msingi kufahamu kinachoendelea katika vikao mbalimbali vya Bunge.
Utafiti wa taasisi hiyo umefanywa katika maeneo tofauti ya Tanzania Bara kupitia mpango wake wa Sauti za Wananchi.
Akitoa
taarifa ya matokeo ya utafiti huo jana jijini Dar e Salaam, Mkurugenzi
Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, alisema suala hilo limeonekana
kutokuungwa mkono na wananchi wengi.
“Asilimia
kubwa ya Watanzania wanapinga uamuzi wa Serikali wa kusitisha matangazo
ya moja kwa moja ya Bunge. Suala hili limeonekana kugusa hisia za watu
wengi na maamuzi haya ya Serikali yakionekana kutoungwa mkono.
“Katika utafiti huu wananchi nane kati ya 10 wanapinga uamuzi wa hali inayodhihirisha kutoungwa mkono kwa hatua hiyo,” alisema Eiyakuze.
Akizungumzia
sababu walizozitoa wananchi wanaotaka matangazo ya Bunge yarushwe moja
kwa moja, Eiyakuze alisema asilimia 46 walisema yanawafanya waweze
kufuatilia utendaji wa wabunge waliowachagua kwa kuwa huko ndio
walikowatuma.
“Asilimia
44 wanasema ni muhimu kwa sababu wananchi wanahaki ya kufahamu
kinachoendelea bungeni, asilimia 29 wanasema matangazo ya moja kwa moja
yalikuwa yanaaminika zaidi kwa watazamaji na wasikilizaji kuona na
kusikia wenyewe kile kinachoendelea tofauti na mfumo wa kurekodi ambapo
kuna baadhi ya mambo yanahaririwa.
“Asilimia
16 walidai kuwa inafursa mwananchi kupata taarifa sahihi badala ya
kuzisoma kwenye magazeti huku asilimia 16 nyingine wakisema inawasaidia
wanachi kufuatilia mijadala ya Bunge kwa wakati”, alisema Eiyakuze.
Pamoja
na hali hiyo mkurugenzi huyo alisema katika utafiti huo asilimia 92 ya
wananchi walisema kuna umuhimu wa vipindi vya Bunge kurushwa moja kwa
moja kupitia Luninga na redio bila kujali gharama zilizoelezwa kuwa ndio
chanzo cha kufikia uamuzi huo.
“Asilimia
88 walisema vipindi vya Bunge virushwe ‘Live’ bila kujali gharama
ukilinganisha na asilimia 12 ambao waliona ni muhimu suala la bajeti
likazingatiwa,” alisema.
Mkurugenzi
huyo alisema asilimia 80 wanaona matangazo ya moja kwa moja kutoka
bungeni ni muhimu kama yalivyo na asilimia 20 wakisema fedha hizo
zitumike kwenye huduma nyinge za jamii.
Akizungumzia
suala la vyombo vya habari vya binafsi kuruhusiwa kurusha matangazo
hayo, Eiyakuze alisema wananchi wanaunga mkono vyombo hivyo kuruhusiwa
iwapo Serikali imeshindwa kumudu gharama.
Utafiti
huo pia umeonesha Watanzinia wanne kati ya kumi wamewahi kuangalia
matangazo ya moja kwa moja kupitia Luninga na sita kati ya kumi
wamesikiliza kupitia redio.
Aidha
utafiti huo umeonyesha zaidi ya nusu ya wananchi walosema wameangalia
au kusikiliza vipindi vya Bunge wamefanya hivyo ndani ya miezi miwili
iliyopita.
Hali ilivyokuwa
Januari
mwaka huu, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye,
alitoa ufafanuzi bungeni kuhusu hatua ya Serikali kusitisha matangazo
hayo kupitia Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC).
Miongoni
mwa sababu alizozieleza ni pamoja na kuwepo kwa gharama kubwa ya Sh
bilioni 4.2 zinazotumika katika uendeshaji wa matangazo hayo ya moja kwa
moja kwa mwaka pia watumishi wa serikali kushabikia Bunge badala ya
kuendelea na kazi ofisini.
Hatua
ya Serikali kusitisha matangazo hayo iliibua mjadala mkubwa bungeni
huku Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, (ACT-Wazalendo) akilitaka
Bunge kusitisha shughuli zake ili kujadili taarifa hiyo ya Serikali.
Siku
chache baadaye kilio hicho cha ukosefu wa fedha za kuonesha matangazo
hayo ya moja kwa moja ambacho kimekuwa kikitolewa na serikali, sasa
kilipata ufumbuzi.
Hatua
hiyo iliyokana na uamuzi wa Mfuko wa Vyombo vya Habari nchini (TMF),
kujitokeza hadharani na kueleza kwamba upo tayari kutoa fedha
zinazohitajika ili kuhakikisha haki ya Mtanzania kupata habari kupitia
TBC haiingiliwi wala kubughudhiwa kwa hoja yoyote.
Endapo
Serikali itakubali ombi hilo, wananchi wataendelea kunufaika na vikao
vya moja kwa moja vya Bunge tofauti na pendekezo la serikali la kunakili
baadhi ya sehemu na kisha kuoneshwa usiku.
No comments:
Post a Comment