Chadema imeondoa mahakamani kesi dhidi ya polisi ya kupinga amri
ya kupiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara, baada ya
kubainika mapungufu ya kisheria katika hati yao ya mashtaka.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hii ofisini kwake jana, Jaji Mohamed Gwae
aliyepangwa kusikiliza shauri hilo alitaja mapungufu ya kisheria
yaliyobainika kwenye hati ya mashtaka ya Chadema kuwa ni pamoja na
kumjumuisha katika hati ya mashtaka Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa
Jeshi la Polisi, Nsato Mssanzya, ambaye kisheria alistahili kufunguliwa
shtaka katika masjala kuu (main registry).
“Baada ya kushauriana na
mawakili wa Chadema kuhusu suala hilo, waliamua kwa hiari yao kuondoa
kesi yao kwa ajili ya kuifanyia marekebisho hati yao ya mashtaka,”
alisema Jaji Gwae.
Akifafanua, Jaji huyo alisema Chadema wana njia
mbili za kurekebisha kasoro hiyo; moja ni kufungua shauri hilo masjala
kuu ya mahakama jijini Dar es Salaam ili kuendelea kumshtaki Kamishina
Mssanzya.
Njia ya pili kwa mujibu wa Jaji Gwae ni Chadema kuendelea na
shauri hilo jijini Mwanza dhidi ya wakuu wa polisi wa wilaya za Maswa,
Kahama na Geita bila kumjumlisha Kamishna Mssanzya.
Akizungumza na
waandishi wa habari muda mfupi baada ya kutoka ofisini kwa Jaji, Wakili
wa Chadema, John Mallya aliyekuwa na mwenzake Paul Kipeja, alisema
shauri hilo halikuanza kusikilizwa jana kutokana na kutokamilika kwa
taratibu za kiofisi za kimahakama.
"Shauri letu bado lipo na tayari
limepangiwa Jaji wa kuisikiliza; ni imani yangu kuwa kesho (leo), hatima
ya kesi yetu itajulikana,” alisema kwa kifupi wakili Mallya bila kutoa
maelezo zaidi.
Juni 10, mwaka huu, Chadema ilifungua kesi mahakamani
kupinga amri ya polisi ya kupiga marufuku maandamano na mikutano ya
hadhara ya kisiasa, kwa kile kilichodaiwa kuwa ni tishio la kiusalama.
Katika hati ya mashtaka iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama
hicho, Freeman Mbowe, Chadema inaiomba mahakama kutamka kuwa amri hiyo
ni batili na utekelezaji wake pia ni batili.
Maombi mengine ni mahakama
kutoa zuio la kimahakama kwa polisi kutotoa amri za aina hiyo tena na
mahakama kuruhusu vyama vya siasa kuendelea na shughuli za kisiasa,
ikiwamo maandamano na mikutano ya hadhara, huku polisi wakiagizwa
kulinda usalama kama sheria inavyoagiza.
No comments:
Post a Comment