Wakati hatua ya upinzani kumsusia Naibu Spika, Dk Tulia Ackson ikiingia
siku ya nane, Kambi ya upinzani imesema leo itawasilisha vipande muhimu
vya hotuba kivuli ya bajeti ambavyo ni vya msingi.
Naibu msemaji
wa kambi hiyo kwa Wizara ya Fedha na Mipango, David Silinde alisema
kutokana na umuhimu wa vipande hivyo ambavyo hakuvitaja, atavisoma kwa
ufupi na kuviwasilisha, kisha kuondoka.
Wabunge wa upinzani
walianza kususia vikao anavyoongoza Dk Tulia Jumanne ya wiki iliyopita,
kufuatia kitendo cha kiongozi huyo kuzuia hoja ya Mbunge wa Arumeru
Mashariki, Joshua Nassari kuhusu kutimuliwa kwa wanafunzi 7,802 wa chuo
kikuu cha Dodoma (Udom).
Jumatatu ya wiki iliyopita Dk Tulia
alizuia hoja ya Nassari akieleza kuwa kutokana na anavyoona sakata hilo
la wanafunzi wa Udom halikuwa la muhimu kusimamisha shughuli za Bunge
kwa wakati huo kwa kuwa Serikali tayari ilishatoa majibu.
Kitendo
hicho kilisababisha wabunge wa upinzani kupinga uamuzi huo jambo
lililosababisha Dk Tulia kuahirisha shughuli za Bunge kabla ya muda huku
Nassari akitolewa bungeni na askari wa Bunge.
Baada ya hatua
hiyo, wabunge wa upinzani walitoka bungeni na kukutana katika ukumbi wa
Msekwa na baadaye Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe
alisema wameazimia kususia vikao vyote vitakavyoongozwa na Dk Tulia, kwa
kuwa hawako tayari kuona demokrasia inaminywa.
Kutokana na hali
hiyo Jumanne ya wiki iliyopita wabunge hao waliingia bungeni kama
kawaida na Dk Tulia alipomaliza tu kusoma dua ya kuliombea Bunge,
walitoka nje hadi kipindi hicho kilipomalizika na Dk Tulia kumwachia
mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge kuongoza ndipo wote waliporudi.
Mbali
na hatua hiyo, Mbunge wa Simanjiro, James Millya kwa niaba ya wabunge
wenzake aliwasilisha hoja kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, akieleza nia
ya kumng’oa Naibu Spika madarakani.
Hoja hiyo imekubaliwa na
Spika Ndugai ambaye juzi katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya
habari na ofisi ya Bunge ilieleza kuwa anakusudia kuiwasilisha kwenye
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iweze kufanyiwa kazi.
Hata
hivyo, wabunge wa CCM juzi walikutana na Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana na kukubaliana kuwapuuza wapinzani, wakisema Naibu
Spika aendelee kuongoza Bunge kwa kuwa hajavunja kanuni yoyote.
Katibu
wa wabunge wa CCM, Jason Rweikiza, alisema, “Kinachofanywa na wabunge
wa upinzani kutoka nje ni uhuni na wananchi waliowachagua wajue wabunge
wao ni wahuni.”
Alisema mbuge mwenye malalamiko dhidi ya mbunge mwenzie au Spika au naibu anajua cha kufanya.
No comments:
Post a Comment