Waziri
mkuu, Kassim Majaliwa amezitaka benki nchini zipitie upya riba zake ili
Watanzania waweze kukopa na kurejesha kwa urahisi.
Amesema riba kubwa zinazotozwa na baadhi ya benki, huduma
zisizokidhi mahitaji na uelewa mdogo wa masuala ya kifedha ni miongoni
mwa changamoto wanazokabiliana nazo wananchi wanapotaka huduma za
kifedha.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Juni 15, 2016) wakati
wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi (COBAT)
mjini Dodoma.
Mkutano huo ulijumuisha wajumbe kutoka mikoa 10 ya Kigoma, Lindi,
Simiyu, Manyara, Katavi, Mbeya, Mwanza, Morogoro, Singida na Dodoma kati
ya mikoa 18 ya Tanzania Bara ambayo bado haina Benki za Wananchi ila
ipo katika hatua za kuanzisha.
Amesema changamoto nyingine ni kutokuwepo kwa taarifa mbalimbali za
sheria na taratibu ambazo zinakwamisha ufanisi wa kiutendaji kwa baadhi
ya taasisi hasa zile zinazolenga kuwahudumia watu wa kipato cha chini.
“Tunahitaji kutafuta njia bora ya kutatua changamoto hizi, na Benki
za Wananchi ni kiungo muhimu katika kushughulikia changamoto
zinazokabili utoaji wa huduma za kifedha.
Waziri Mkuu amesema ni muhimu kuanzisha Benki za Wananchi katika
kila Mkoa ili kuweza kusambaza huduma hizo karibu zaidi na walengwa,
hali ambayo itasaidia kupunguza umasikini kupitia ukuaji wa shughuli za
kiuchumi.
Amesema Serikali itaangalia uwezekano wa kuiwezesha mikoa ambayo
itaonyesha ari zaidi ya kuanzisha benki zao na akatoa wito waandae
mikakati ya kuhamasisha wananchi ili wakusanye mitaji ya kutosha.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa COBAT, Bibi Elizabeth Makwabe
amesema Jumuiya yao ilianzishwa mwaka 2006 ikiwa na wanachama saba na
sasa hivi wamefikia 10 huku wananchi wanaowahudumiwa na benki hizo ni
zaidi ya milioni mbili.
Amesema Jumuiya za Benki ya Wananchi inakabiliwa na changamoto
mbalimbali zikiwemo mfumo hafifu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(TEHAMA) pamoja na ufinyu wa mitaji.
No comments:
Post a Comment